Dar es Salaam.
Serikali imetangaza majina ya wanafunzi 18,754 waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya ualimu vilivyo chini yake ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 1,659 ikilinganishwa na 17,095 waliochaguliwa mwaka jana.
Kati ya wanafunzi hao, 11,806 wamechaguliwa kusomea ngazi ya cheti (Grade A) na 6,948 watasoma katika ngazi ya stashahada.
Wanafunzi 363 wamechaguliwa kusoma elimu maalumu kwa ngazi ya cheti huku 57 wakisoma elimu hiyo kwa ngazi ya stashahada.
Akizungumza na mwandishi wetu jana, Msemaji wa
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ntambi Bunyazu alisema wanafunzi
wanatakiwa kuripoti kwenye vyuo walivyopangiwa kuanzia Agosti 15, mwaka
huu.
“Usajili utafungwa Agosti 25 saa 12:00 jioni,
‘Joining instructions’ (fomu ya maelekezo ya kujiunga) zitatumwa kwa
wahusika kupitia anuani zao.... fomu hizi pia zinapatikana kwenye tovuti
ya Wizara ya Elimu na mafunzo ya Ufundi,” alisema.
Taarifa ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
iliyotolewa baadaye jana ilisema kuwa wanafunzi waliochaguliwa
wanatakiwa kufika vyuoni wakiwa na vyeti halisi vya kidato cha nne na
cha sita vinavyotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) , ada
ya muhula wa kwanza Sh100,000 au Sh200,000 kwa mwaka.
Wanatakiwa kuwa na “Sare ya chuo kulingana na
maelekezo ya chuo husika, fedha za tahadhari chuoni na matumizi
binafsi,” inasema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inaeleza pia kuwa wakuu wa vyuo
wanatakiwa kuhakikisha wanafunzi wanaosajiliwa ni wale waliopo kwenye
orodha iliyotolewa na wizara na si vinginevyo.
Wengi wa wanafunzi hawa ni wale waliohitimu kidato
cha nne mwaka 2012 na kidato cha sita mwaka huu. Kwa upande wa wale wa
kidato cha nne, matokeo yaliyotangazwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi yalionyesha kuwa watahiniwa 159,609 wa shule walifaulu kwa daraja
la kwanza mpaka la nne.
Inaonyesha pia kuwa kwa upande wa Tanzania Bara,
wanafunzi 34,599 walifaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu na kati
yake waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi
walikuwa ni 34,213.
Kwa upande wa matokeo ya kidato cha sita mwaka
huu, watahiniwa waliofaulu mtihani huo walikuwa ni 44,366 kati yao
40,242 wakiwa ni wa shule. Matokeo hayo yanaonyesha pia kuwa, watahiniwa
35,880 ndiyo waliofaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu.
Kwa mujibu wa Kitabu cha Takwimu cha Wizara ya
Elimu (Best), mwaka 2012 wanafunzi 17,095 walichaguliwa kujiunga na vyuo
mbalimbali vya ualimu nchini.
No comments:
Post a Comment