Wednesday, 31 July 2013

"WAPIGWE TU" YA MIZENGO PINDA ITAMFIKISHA KORTINI



KAULI ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ya kubariki vyombo vya dola kuendeleza kipigo kwa raia wanaokaidi amri imechukua sura mpya baada ya Kituo cha Sheria na Haki za Bindamu (LHRC) kutangaza kumburuza mahakamani wiki hii kutokana na kushindwa kufuta kauli yake.


Juni 20, mwaka huu, wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo bungeni, Waziri Mkuu, Pinda, alivitaka vyombo vya dola kuendelea kuwapiga raia, akisema kuwa hakuna namna nyingine kwani serikali imechoka.


Kauli hiyo imekuwa ikipingwa na wananchi, mashirika ya kutetea haki za binadamu na wanasiasa wakimtaka Waziri Mkuu, Pinda, kuifuta kwa kuomba radhi, wakidai kuwa inachochea uvunjifu wa sheria.


Akitangaza kusudio la kituo hicho kufungua kesi dhidi ya Pinda, Mkurugenzi wa maboresho na utetezi, Harold Sungusia, alisema hadi jana walikuwa tayari wameandaa kusudio la shtaka lao.


Alisema kuwa kisheria kilichowafanya kufikia uamuzi huo ni kutokana na waziri mkuu huyo kukiuka Katiba ya nchi inayozungumzia usawa mbele ya sheria.


“Kitendo alichofanya waziri mkuu cha kuwaruhusu polisi kupiga wananchi hakikubaliki hata kidogo na walitegemea kwamba angeomba radhi kutokana na kauli yake hiyo tangu alivyoshinikizwa kufanya hivyo na makundi mbalimbali.


“Badala yake ameendelea kuwa kimya licha ya mkubwa wake, Rais Jakaya Kikwete, hivi karibuni kukiri kwamba mtendaji wake huyo aliteleza,” alisema.


Sungusia aliongeza kuwa Alhamisi wiki hii wataweka bayana kwa waandishi wa habari ni wapi kesi hiyo itafunguliwa.


Pinda alitoa kauli hiyo tata ambayo imehojiwa na wengi wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM) aliyehoji kama serikali iko tayari kutoa tamko kuhusu vurugu zilizotokea jijini Arusha, Mtwara na maeneo mengine pamoja na hatua ya vyombo vya dola kutumia nguvu.


Katika majibu yake Pinda alisema kuwa suala la amani linawagusa wote, kwamba jukumu ni kwa viongozi wa kisiasa. Alifafanua kuwa kama viongozi wa kisiasa hawatafika mahali wakakubaliana bila kujali vyama vyao nchi itafika pabaya.


Pinda alifafanua kuwa kwa upande wa serikali lazima wahakikishe kwamba wale wote wanaojaribu kuvunja amani kwa namna yoyote ile kazi waliyonayo ni kupambana kweli kweli kwa njia zozote zinazostahili.


“Mimi naomba sana Watanzania, maana kila juhudi zinazoonekana zinaelekea huko, tunapata watu wengine wanajitokeza kuwa mara unajua…unajua. Acheni serikali itimize wajibu wake, kwa sababu jambo hili ni la msingi na wote tulilinde kwa nguvu zetu zote.


“Mheshimiwa Mangungu umeanza vizuri lakini hapa unasema vyombo vya dola vinapiga watu. Ukifanya fujo unaambiwa usifanye hiki, ukaamua wewe kukaidi, utapigwa tu,” alisema.


Waziri mkuu aliongeza kuwa hakuna namna nyingine, maana lazima watu wakubaliane na serikali kwamba nchi hii wanaiendesha kwa misingi ya kisheria.


“Sasa kama wewe umekaidi, hutaki, unaona kwamba ni imara zaidi, wewe ni jeuri zaidi, watakupiga tu, na mimi nasema wapigwe tu, maana hakuna namna nyingine, tumechoka,” alisema

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment