Tuesday, 20 August 2013

Picha na habari kamili kuhusu vurugu zilizotokea jijini mwanza leo


 

MAANDAMANO ya amani yaliyokuwa yameandaliwa na chama cha demokrasia na maendeleo(chadema) yamegeuka shubiri kwa wakazi wa jiji la Mwanza baada ya kuibuka mapambano makali baina ya waandamanaji hao na jeshi la polisi mkoani Mwanza na kusababisha polisi kutumia nguvu kuwatawanya wafuasi wa chama hicho.

 

Maandamano hayo ya amani ambayo yalianzia katika eneo la Buzuruga nje kidogo ya jiji la Mwanza yalikuwa  yakiongozwa na wabunge Highness Kiwia wa Ilemela  pamoja na Ezekiel Wenje kuelekea katika viwanja vya Furahisha na yalilenga kumshinikiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Ernest Ndikilo kutoa barua zinazodaiwa kuandikwa na ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi kuwarejesha madiwani watatu waliotimuliwa katika Manispaa ya Ilemela kutokana na kushindwa kuhudhuria vikao vitatu mfululizo.

 

Polisi wenye silaha pamoja na askari kanzu walianza kutanda katika eneo hilo la Furahisha wakiongozwa na Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Mwanza RCO Konyo ambaye alikuwa akitumia gari lenye namba za usajili DK 068EXV aina ya Toyota Land Cruiser

 

Maandamano hayo ambayo awali yalionekana kana kwamba yangelimalizika salama yaliwasili katika viwanja vya Furahisha majira ya saa 5.38 huku yakiongozwa na gari la polisi lenye namba za usajili za nchi ya Uganda  779 UAG likiwa nimesheheni polisi wenye silaha nzito ikiwa ni pamoja na mabomu ya machozi na bunduki pamoja na askari kadhaa ambao walikuwa katikati ya maandamano hayo.

 

Baada ya maandamano hayo kuwasili katika viwanja vya Furahisha kwa amani,waandamani hao ambao walikuwa na mabango mbalimbali yaliyosomeka kuwa :‘Matata hatutaki uendelee kuwa Meya wa Ilemela rudia kazi yako ya awali,.... na jingine Jaji Sumari tumechoka kuahirisha mara kwa  mara kesi dhidi ya Matata ....na jingine  lililosomeka kuwa RD Ndikilo tunahitaji barua za kurejeshwa kwa madiwani wetu.

 

Hata hivyo tofauti na ilivyokuwa imetangazwa kuwa maandamano hayo ya amani yangelipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Ernest Ndikilo,hakukuwa na kiongozi yoyote wa Serikali ambaye alikuwepo uwanjani hapo kupokea maandamano hayo.

 

Kufuatia kutoonekana kwa kiongozi yoyote wa Serikali,viongozi wa chadema pamoja na wabunge wao walikutana kwa faragha kwa dakika kadhaa kwa ajili ya kujua hatima ya maandamano hayo ambapo Mbunge wa Nyamagana Ezekiel Wenje alipanda jukwaani saa 6.45 na kuwaeleza maelfu ya waandamanaji kuwa wameamua kumtuma Mbunge wa Ilemela Highnes Kiwia kwenda ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kuchukua majibu kwa ajili ya kuwaletea wananchi walioandamana juu ya hatima ya madiwani hao.

 

Hata hivyo saa moja baadae Mbunge huyo alisimama jukwani na wakuwaeleza waandamani hao kuwa simu ya Mbunge Kiwia ilikuwa haipatikani hivyo kuwataka kuandamana kwenda kwa Mkuu wa mkoa wa Mwanza kujua kulikoni na hapo ndipo hali ya hewa ilipochafuka.

 

Jeshi la polisi baada ya kuona wandamanaji hao wameanza kuelekea katika ofisi za Mkuu wa mkoa liliwataka kutawanyika ambapo waandamanaji hao walikaidi ndipo jeshi la polisi lilipoamua kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wafuasi hao.

 

Vurugu hizo ambazo zilianza majira ya saa 7.30 zilisababisha kufungwa kwa baadhi ya barabara kutokana na waandamanji hao kuweka vizuizi vya mawe na kuchoma matairi,ambapo pia maduka na ofisi mbalimbali zililazimika kufungwa kwa muda kupisha vurugu hizo.

 


Baadhi ya wananchi ambao walikuwa wakitumia usafiri wa umma walionekana wakishuka kupitia katika madirisha ya magari hayo na kukimbia kwa hofu ya kujeruhiwa na mabomu pamoja na mawe ambayo yalikuwa yakirushwa na waandamanji hao kwa jeshi la polisi.

 

MKUU WA MKOA WA MWANZA ALONGA.

Mkuu wa mkoa wa Mwanza akizungumza na Mbunge Kiwia pamoja na viongozi wa chadema ofisini kwake alisema kuwa ameshangazwa na uvumi huo kuwa ofisi yake imekalia barua za kurejeshwa kwa madiwani Abubakar Kapera(Nyamanoro),Dan Kahungu(Kirumba) pamoja na Marietha Chenyenge(Ilemela).

 

RC Ndikilo alisema kuwa Serikali imekuwa ikifanya kazi zake kwa maandishi na sio kwa kufuata maneno ya mtaani na kueleza kuwa hana barua yoyote toka ofisi ya Waziri Mkuu inayomualifu kuhusu kuwarejesha madiwani hao baada ya kukata rufaa.

 

“We Mbunge kuna siku ulinipigia simu ukiniuliza juu ya kuwepo kwa barua hizo nami nilikujibu kuwa kwa kuwa uko hapo Bungeni Dodoma ambapo pia kuna ofisi ya Waziri Mkuu nilikujibu kuwa ni muhimu ukawaona viongozi wakuu wa Tamisemi ikiwa ni pamoja na Waziri Mkuu,pia nilikushauri kuwa wakupe japo nakala ya barua hiyo”,alisema RC Ndikilo.

 

“Lakini cha kushangaza nimekuwa nikisikia maneno ya ajabu kuwa nimeficha barua za madiwani hao,ikumbukwe kuwa madiwnai hao hawakukata rufaa kwangu bali walikata rufaa ngazi ya juu kabisa,ili kukata mzizi wa fitina naomba kati ya tarehe 26 hadi 27 wewe Mbunge pamoja na mimi twende TAMISEMI kukutana na viongozi ili kukata mzizi wa fitina na tuje tuwaeleze wananchi ukweli uliopo”,alisema RC Ndikilo.

 

Kuhusu suala la Meya Henry Matata kutoondolewa madarakani RC Ndikilo alisema kuwa hawezi kulizungumzia suala hilo kwa kuheshimu mamlaka ya mahakama na kuwataka chadema kuvuta subira hadi pale mahakama itakapotoa maamuzi yake.

 

KAULI YA MBUNGE KIWIA.

Akizungumza katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Kiwia alisema kuwa waliamua kuitisha maandamano hayo kutokana na kuelezwa na Waziri Hawa Ghasia kuwa tayari barua hizo zimeishatumwa mkoani Mwanza.

 


“Mheshimiwa Mkuu wa mkoa hawa madiwani waliosimamishwa  ni wawakilishi wa wananchi,wamekaa nje kwa miezi saba sasa na uchaguzi wa Meya haukuwa halali ndio maana tuliamua kuitisha maandamano kwa ajili ya kuhakikisha madiwani hawa wanarejeshwa.

 


RPC MANGU.

Akizungumza kwa simu juu ya kutokea kwa vurugu zilizosababisha kupigwa  kwa mabomu ya machozi,Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Ernest Mangu alisema kuwa polisi walifanikiwa kudhibiti vurugu hizo na hadi sasa hawezi kusema ni wananchi wangapi ambao walikamatwa kuhusu vurugu hizo.




















No comments:

Post a Comment