Tuesday, 1 July 2014

TRA waanza rasmi ukaguzi na urasimishaji wa kazi za muziki na filamu


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza kuanza rasmi ukaguzi na urasimishaji wa kazi za muziki na filamu kwa kubandika stika maalum kwenye kazi za wasanii hao.
Taasisi za serikali zilizopewa jukumu la kurasimisha kazi za sanaa ya muziki na filamu zimeanza kukagua na kukamata kazi zote ambazo hazina sifa ya kuuzwa ndani au kupelekwa nje ya nchi. 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TRA kwa kuzingatia sheria ya ushuru wa bidhaa iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012 na kupitishwa kwa kanununi zake mwaka 2013, inamtaka kila mfanyabiashara wa kazi za muziki na filamu kuhakikisha kuwa bidhaa yake ina stempu ya ushuru wa bidhaa inayotolewa na TRA kabla ya kusambazwa.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa wasanii wote wa muziki wanapaswa kupitia hatua zote za awali kwa kuipeleka kazi yao BASATA, COSOTA kabla ya kuifikisha TRA kwa ajili ya kununua stempu/stika maalum ya utambulisho wa ushuru.
Kwa wasanii wa filamu wanapaswa kupitisha kazi zao kwenye bodi ya filamu na COSOTA kabla ya kufika TRA kununua stika.
Imeeleza kuwa zoezi hilo litafanyika kwa kazi zote za ndani na za nje ya nchi na kwamba zitatofautiana rangi tu za stempu/stika zitakazoitambulisha.
-Filamu kutoka nje ya nchi-rangi ya kijani (green)
-Muziki toka nje ya nchi –rangi bluu (blue)
=Filamu zinazotengenezwa ndani ya nchi-Zambarau (violet)
-Muziki wa ndani ya nchi –rangi ya pink
“Stempu hizi zitapatikana ofisi za idara ya fedha, makao makuu TRA. Kila kazi yaani CD, DVD au kanda zitatolewa stempu mbili zenye namba moja katika mtiririko maalum wa namba (serial number). Stempu moja hubandikwa katika kasha na nyingne kwenye CD/DVD au Kanda. Utaratibu unamtaka mhusika anaehitaji stempu kuwasilisha maombi tofauti kwa kila kazi husika. Hairuhusiwi kuwekwa stempu zilizoombwa kwa ajili ya kazi moja kwenye kazi nyingine hata kama kazi hizo zimetolewa na mzalishaji au msambazaji mmoja.” Inaeleza taarifa hiyo.

No comments:

Post a Comment