Wednesday 31 July 2013

CHADEMA HAINA UBAVU WA KUMKATAA TENDWA


OFISI ya Msajili wa Vyama vya Siasa, imesema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hakina ubavu wa kumkataa au kutomtambua John Tendwa kuwa ndiye msajili wa vyama vya siasa nchini.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasai, Rajab Baraka alipozungumza na MTANZANIA kuhusu kauli iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa aliyedai chama hicho hakimtambui John Tendwa kuwa ndiye msajili wa vyama vya siasa.

Katika madai yake Dk. Slaa alidai Tendwa anakipendelea CCM katika kutoa haki ya demokrasia na hatendi haki kama mlezi wa vyama vyote vya siasa nchini.

Dk. Slaa alisema hayo wiki iliyopita alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari na kusisitiza hata katika barua zao za mawasiliano kwenda kwa ofisi ya msajili chama hicho hakitumii jina la John Tendwa.

Kwa mujibu wa Dk. Slaa, Chadema kinaitambua ofisi ya Msajili wa Vyama tu lakini hakimtambui Tendwa kuwa ndiye msajili wa vyama vya siasa nchini.

“Hatumpelekei hata barua huyu hatunzi sheria siyo mtu wa kulea vyama ni mlezi wa chama kimoja, hayuko serious na hatushirikiani naye mpaka aondoke madarakani.

“Tukiandika barua hatuweki jina lake lakini tunaitambua ofisi yake, hata yeye mwenyewe analijua hilo na akijibu barua zetu haweki jina lake,” alidai Dk. Slaa.

Akijibu hoja hizo, Naibu Msajili alisema Chadema hawana ubavu wa kutomtambua Tendwa kwa sababu amewekwa kisheria na ofisi yake ipo kisheria.

Alisisitiza Tendwa ataendelea kuwa mlezi wa vyama vyote na siyo chama kimoja kama inavyodaiwa na kuvitaka vyama vyote kuheshimu sheria iliyomuweka madarakani msajili huyo.


Mtanzania.

TANZANIA YAMJIBU RAIS KAGAME....YADAI IPO TAYARI KWA LOLOTE NA AKITHUBUTU ITAMCHAPA KAMA MTOTO

SERIKALI ya Tanzania imeipa onyo kali nchi ya Rwanda ikiitaka isijaribu kuota ndoto za kuishambulia kijeshi, vinginevyo itajibu mapigo kwa nguvu zote na kuhakikisha kuwa imeichakaza.


Kauli hiyo ya kwanza nzito imetolewa jana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Kimataifa kufuatia taarifa ya matamshi makali yanayodaiwa kutolewa na Rais Paul Kagame wa Rwanda, dhidi ya Rais Jakaya Kikwete na kutishia kuishambulia Tanzania.


Akizungumza na Tanzania Daima jana jijini Dar es Salaam, Msemaji wa wizara hiyo, Mkumbwa Ally, alisema ingawa Serikali ya Tanzania hadi sasa inajua haina ugomvi wowote na Rwanda, lakini amekiri kuwapo kwa kile alichokiita ‘kupishana lugha’ kwa Rais Jakaya Kikwete na Paul Kagame.


Mkumbwa alikiri Serikali ya Tanzania kunasa matamshi yanayodaiwa kutolewa na Rais Kagame katika moja ya hotuba zake aliyoitoa Juni 30, nchini kwake wakati akihutubia katika hafla moja ya vijana.


Kwa mujibu wa hotuba hiyo, ambayo kwa wiki sasa imesambazwa katika baadhi ya mitandao ya kijamii, Kagame anadaiwa kusikika akitoa matamshi ya vitisho dhidi ya Rais Kikwete, kwamba anamsubiri katika wakati aujuao na kumchapa.


Baadhi ya maneno yanayodaiwa Rais Kagame aliwaambia vijana waliokutana katika mkutano wao uliojulikana kama ‘Youth Konnect’ na kufadhiliwa na mke wake, Janet Kagame, yanasema: “Huyu mtu mliyemsikia akiwa upande wa Interahamwe na FDLR na akashauri majadiliano….majadiliano?”


Aidha, Kagame anadaiwa kusema kuwa hatakuwa tayari kujadili jambo hilo, isipokuwa atamsubiri Rais Kikwete sehemu muafaka na ‘kumtandika’.

“Sitapoteza muda wangu kumjibu Kikwete, inajulikana maana kuna mahali hataweza kuvuka…haiwezekani,” alikaririwa akisema Rais Kagame, akilenga kumtisha Rais Kikwete.


Mbali na Kagame, baadhi ya viongozi kadhaa wa serikali ya Rwanda wamekuwa wakimshambulia Rais Kikwete wakimpachika majina ya kejeli ya; “Rais mhurumia magaidi, wauaji wa kimbari, mkorofi na mwenye dharau.”


Mkumbwa hata hivyo alisema Serikali ya Tanzania haina sababu ya kuingia katika vita na Rwanda, kwa sababu tu ya ushauri alioutoa Rais Kikwete wa kuitaka ikutane na wapinzani wake wanaoishi ndani ya nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kujadiliana kuhusu amani ya nchi za Maziwa Makuu.


Alisema msimamo wa Tanzania utabaki kuwa uleule wa kuitaka nchi hiyo ikubali kukaa meza moja na wapinzani wake, ili kumaliza migogoro inayoendelea katika nchi hizo za maziwa makuu, ambao unaungwa mkono na jumuiya ya kimataifa na SADC.

“Unajua mgogoro wa DRC na Rwanda hauwezi kumalizika bila ya nchi hizo kukaa meza moja na wapinzani wao ili kupata suluhu ya kudumu,” alisema Mkumbwa.


Aliwataka Watanzania kuwa watulivu na kuendelea na kazi zao kama kawaida, kwani serikali yao iko makini katika kulinda mipaka yake.

Chanzo cha mzozo
Msuguano baina ya nchi hizi mbili ulianza siku chache tu baada ya kumalizika kwa kikao cha viongozi wa nchi za Maziwa Makuu na ambacho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon, chini ya uenyekiti wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni.

Rais Kikwete wakati akimtaarifu Rais Museveni kile walichokuwa wamekijadili katika kikao hicho kwa vile aliketi kwa muda kwa kuwa alichelewa kuwasili, alisema ni vema serikali za Rwanda na Uganda zifungue mlango wa mazungumzo na waasi wao na akaanza kutaja majina ya vikundi vya uasi vya nchi hiyo vilivyopo nchini DRC.

Habari zinasema kauli ya Rais Kikwete iliungwa mkono na Rais Museveni akisema: “Bila mazungumzo hatutafika popote pale”.  


Hata hivyo, matamshi hayo yalijibiwa kwa ukali na serikali ya Rwanda, kiasi cha kumlazimu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kutoa tamko bungeni.


Kwa kauli yake, Membe alisema serikali ilikuwa imeshangazwa na shutuma hizo za Rwanda kwani halikuwa jambo baya kutoa ushauri uliolenga kuleta mapatano na kuepusha umwagaji zaidi wa damu wa wananchi. 

Akaongeza kuwa, ilikuwa ni wajibu wa Serikali ya Rwanda kuupokea ama kuukataa, na wala si kutoa maneno ya kejeli na vitisho.

Kauli ya Zitto
Akizungumzia kauli hiyo ya vitisho, mwanasiasa machachari hapa nchini na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Zitto Kabwe, alisema ushauri wa Rais Kikwete kwa Rwanda ulikuwa wa busara mno na akashangaa kuona nchi hiyo jirani ikitoa vitisho, kejeli, dharau na ukosefu wa adabu kwa Kikwete.
 
Katika moja ya tamshi lake alilolitoa jana katika mitandano ya kijamii, Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA) alisema Marekani wanaongea na waasi wa kundi la Taliban, hivyo hakuna dhambi kwa Rwanda pia kufanya hivyo.

“Pia kama hutaki ushauri si unakataa tu, sasa kuanza kurushiana maneno ya nini tena? Hutaki ushauri basi. 

Maneno ya kila siku ya nini? Tangu Kikwete amesema kule Addis, hajasema tena. Membe (waziri) akajibu Dodoma Tanzania haijasema tena. Kigali inasema mambo haya kila siku kwa ajili ya nini?


“Taliban na Al Qaeda si wale wale? Wale watoto waliozaliwa mwaka 1994 na wakimbizi wa Kihutu waliopo Kongo nao ni wauaji? Tufikiri vizuri mambo haya. Kuna ‘genociders’ wasakwe, wakamatwe wahukumiwe. Kuna watu wana haki kabisa ya kutaka kushiriki kwenye siasa za Rwanda na wanazuiwa, wameshika silaha. Hawa lazima wakae meza moja wakubaliane,” alisema Zitto.

Mwanasiasa huyu alisema kwa sasa serikali za nchi hizo mbili zinatakiwa kuingia katika vita ya kupambana na kuondoa umasikini wa watu wake na si vita ya mtutu wa bunduki.

“Busara itumike kwa viongozi ‘neutral’ kama Uhuru Kenyatta kuwaweka pamoja Kagame na Kikwete wamalize tofauti zao. Haya maneno hayana maana yoyote,” alisema.

Alisema vita haitamuumiza Rais Kagame wala Rais Kikwete na familia zao, bali itaumiza wananchi wa kawaida wa mikoa ya Kagera na Kigoma na mikoa ya mpakani ya Rwanda.


“Vita itaturudisha nyuma sana kwenye juhudi za maendeleo. Vita itazima harakati za kujenga demokrasia nchini.  Busara itumike tu,” alisema Zitto.

Tanzania Daima

Wanaokwenda ualimu

Dar es Salaam.

Serikali imetangaza majina ya wanafunzi 18,754 waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya ualimu vilivyo chini yake ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 1,659 ikilinganishwa na 17,095 waliochaguliwa mwaka jana.
Kati ya wanafunzi hao, 11,806 wamechaguliwa kusomea ngazi ya cheti (Grade A) na 6,948 watasoma katika ngazi ya stashahada.
Wanafunzi 363 wamechaguliwa kusoma elimu maalumu kwa ngazi ya cheti huku 57 wakisoma elimu hiyo kwa ngazi ya stashahada.
Akizungumza na mwandishi wetu jana, Msemaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ntambi Bunyazu alisema wanafunzi wanatakiwa kuripoti kwenye vyuo walivyopangiwa kuanzia Agosti 15, mwaka huu.
“Usajili utafungwa Agosti 25 saa 12:00 jioni, ‘Joining instructions’ (fomu ya maelekezo ya kujiunga) zitatumwa kwa wahusika kupitia anuani zao.... fomu hizi pia zinapatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Elimu na mafunzo ya Ufundi,” alisema.
Taarifa ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliyotolewa baadaye jana ilisema kuwa wanafunzi waliochaguliwa wanatakiwa kufika vyuoni wakiwa na vyeti halisi vya kidato cha nne na cha sita vinavyotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) , ada ya muhula wa kwanza Sh100,000 au Sh200,000 kwa mwaka.
Wanatakiwa kuwa na “Sare ya chuo kulingana na maelekezo ya chuo husika, fedha za tahadhari chuoni na matumizi binafsi,” inasema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inaeleza pia kuwa wakuu wa vyuo wanatakiwa kuhakikisha wanafunzi wanaosajiliwa ni wale waliopo kwenye orodha iliyotolewa na wizara na si vinginevyo.
Wengi wa wanafunzi hawa ni wale waliohitimu kidato cha nne mwaka 2012 na kidato cha sita mwaka huu. Kwa upande wa wale wa kidato cha nne, matokeo yaliyotangazwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi yalionyesha kuwa watahiniwa 159,609 wa shule walifaulu kwa daraja la kwanza mpaka la nne.
Inaonyesha pia kuwa kwa upande wa Tanzania Bara, wanafunzi 34,599 walifaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu na kati yake waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi walikuwa ni 34,213.
Kwa upande wa matokeo ya kidato cha sita mwaka huu, watahiniwa waliofaulu mtihani huo walikuwa ni 44,366 kati yao 40,242 wakiwa ni wa shule. Matokeo hayo yanaonyesha pia kuwa, watahiniwa 35,880 ndiyo waliofaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu.
Kwa mujibu wa Kitabu cha Takwimu cha Wizara ya Elimu (Best), mwaka 2012 wanafunzi 17,095 walichaguliwa kujiunga na vyuo mbalimbali vya ualimu nchini.

"WAPIGWE TU" YA MIZENGO PINDA ITAMFIKISHA KORTINI



KAULI ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ya kubariki vyombo vya dola kuendeleza kipigo kwa raia wanaokaidi amri imechukua sura mpya baada ya Kituo cha Sheria na Haki za Bindamu (LHRC) kutangaza kumburuza mahakamani wiki hii kutokana na kushindwa kufuta kauli yake.


Juni 20, mwaka huu, wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo bungeni, Waziri Mkuu, Pinda, alivitaka vyombo vya dola kuendelea kuwapiga raia, akisema kuwa hakuna namna nyingine kwani serikali imechoka.


Kauli hiyo imekuwa ikipingwa na wananchi, mashirika ya kutetea haki za binadamu na wanasiasa wakimtaka Waziri Mkuu, Pinda, kuifuta kwa kuomba radhi, wakidai kuwa inachochea uvunjifu wa sheria.


Akitangaza kusudio la kituo hicho kufungua kesi dhidi ya Pinda, Mkurugenzi wa maboresho na utetezi, Harold Sungusia, alisema hadi jana walikuwa tayari wameandaa kusudio la shtaka lao.


Alisema kuwa kisheria kilichowafanya kufikia uamuzi huo ni kutokana na waziri mkuu huyo kukiuka Katiba ya nchi inayozungumzia usawa mbele ya sheria.


“Kitendo alichofanya waziri mkuu cha kuwaruhusu polisi kupiga wananchi hakikubaliki hata kidogo na walitegemea kwamba angeomba radhi kutokana na kauli yake hiyo tangu alivyoshinikizwa kufanya hivyo na makundi mbalimbali.


“Badala yake ameendelea kuwa kimya licha ya mkubwa wake, Rais Jakaya Kikwete, hivi karibuni kukiri kwamba mtendaji wake huyo aliteleza,” alisema.


Sungusia aliongeza kuwa Alhamisi wiki hii wataweka bayana kwa waandishi wa habari ni wapi kesi hiyo itafunguliwa.


Pinda alitoa kauli hiyo tata ambayo imehojiwa na wengi wakati akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu (CCM) aliyehoji kama serikali iko tayari kutoa tamko kuhusu vurugu zilizotokea jijini Arusha, Mtwara na maeneo mengine pamoja na hatua ya vyombo vya dola kutumia nguvu.


Katika majibu yake Pinda alisema kuwa suala la amani linawagusa wote, kwamba jukumu ni kwa viongozi wa kisiasa. Alifafanua kuwa kama viongozi wa kisiasa hawatafika mahali wakakubaliana bila kujali vyama vyao nchi itafika pabaya.


Pinda alifafanua kuwa kwa upande wa serikali lazima wahakikishe kwamba wale wote wanaojaribu kuvunja amani kwa namna yoyote ile kazi waliyonayo ni kupambana kweli kweli kwa njia zozote zinazostahili.


“Mimi naomba sana Watanzania, maana kila juhudi zinazoonekana zinaelekea huko, tunapata watu wengine wanajitokeza kuwa mara unajua…unajua. Acheni serikali itimize wajibu wake, kwa sababu jambo hili ni la msingi na wote tulilinde kwa nguvu zetu zote.


“Mheshimiwa Mangungu umeanza vizuri lakini hapa unasema vyombo vya dola vinapiga watu. Ukifanya fujo unaambiwa usifanye hiki, ukaamua wewe kukaidi, utapigwa tu,” alisema.


Waziri mkuu aliongeza kuwa hakuna namna nyingine, maana lazima watu wakubaliane na serikali kwamba nchi hii wanaiendesha kwa misingi ya kisheria.


“Sasa kama wewe umekaidi, hutaki, unaona kwamba ni imara zaidi, wewe ni jeuri zaidi, watakupiga tu, na mimi nasema wapigwe tu, maana hakuna namna nyingine, tumechoka,” alisema

Tanzania Daima