Wednesday 31 July 2013

Wanaokwenda ualimu

Dar es Salaam.

Serikali imetangaza majina ya wanafunzi 18,754 waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya ualimu vilivyo chini yake ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 1,659 ikilinganishwa na 17,095 waliochaguliwa mwaka jana.
Kati ya wanafunzi hao, 11,806 wamechaguliwa kusomea ngazi ya cheti (Grade A) na 6,948 watasoma katika ngazi ya stashahada.
Wanafunzi 363 wamechaguliwa kusoma elimu maalumu kwa ngazi ya cheti huku 57 wakisoma elimu hiyo kwa ngazi ya stashahada.
Akizungumza na mwandishi wetu jana, Msemaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ntambi Bunyazu alisema wanafunzi wanatakiwa kuripoti kwenye vyuo walivyopangiwa kuanzia Agosti 15, mwaka huu.
“Usajili utafungwa Agosti 25 saa 12:00 jioni, ‘Joining instructions’ (fomu ya maelekezo ya kujiunga) zitatumwa kwa wahusika kupitia anuani zao.... fomu hizi pia zinapatikana kwenye tovuti ya Wizara ya Elimu na mafunzo ya Ufundi,” alisema.
Taarifa ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliyotolewa baadaye jana ilisema kuwa wanafunzi waliochaguliwa wanatakiwa kufika vyuoni wakiwa na vyeti halisi vya kidato cha nne na cha sita vinavyotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) , ada ya muhula wa kwanza Sh100,000 au Sh200,000 kwa mwaka.
Wanatakiwa kuwa na “Sare ya chuo kulingana na maelekezo ya chuo husika, fedha za tahadhari chuoni na matumizi binafsi,” inasema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inaeleza pia kuwa wakuu wa vyuo wanatakiwa kuhakikisha wanafunzi wanaosajiliwa ni wale waliopo kwenye orodha iliyotolewa na wizara na si vinginevyo.
Wengi wa wanafunzi hawa ni wale waliohitimu kidato cha nne mwaka 2012 na kidato cha sita mwaka huu. Kwa upande wa wale wa kidato cha nne, matokeo yaliyotangazwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi yalionyesha kuwa watahiniwa 159,609 wa shule walifaulu kwa daraja la kwanza mpaka la nne.
Inaonyesha pia kuwa kwa upande wa Tanzania Bara, wanafunzi 34,599 walifaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu na kati yake waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano na vyuo vya ufundi walikuwa ni 34,213.
Kwa upande wa matokeo ya kidato cha sita mwaka huu, watahiniwa waliofaulu mtihani huo walikuwa ni 44,366 kati yao 40,242 wakiwa ni wa shule. Matokeo hayo yanaonyesha pia kuwa, watahiniwa 35,880 ndiyo waliofaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu.
Kwa mujibu wa Kitabu cha Takwimu cha Wizara ya Elimu (Best), mwaka 2012 wanafunzi 17,095 walichaguliwa kujiunga na vyuo mbalimbali vya ualimu nchini.

No comments:

Post a Comment