Thursday, 24 October 2013

MAMA KANUMBA ATAKA MCHUNGAJI AKAMATWE


by zangii ze icon
Stori: zangii koroboy
SIKU chache baada ya mchungaji aliyejitambulisha kwa jina moja la Mayanga kuibuka na kudai ndiye amewaua Steven Kanumba na Hussein Mkiety ‘Sharo Milionea’, mama mzazi wa Kanumba, Flora Mtegoa ametaka jamaa huyo akamatwe mara moja na kufikishwa kwenye vyombo vya dola.
Mchungaji Mayanga (mwenye kipaza sauti) akitoa ushuhuda kuwa ndiye aliyewaua Steven Kanumba na Hussein Mkiety ‘Sharo Milionea’.
Mbali na kudai kumuua Kanumba na Sharo, Mchungaji Mayanga alidai kabla ya kuokoka kuwa alihusika na vifo vya watu milioni 605 wakiwemo wasanii wa Kundi la Five Stars wapatao 14 na mwanamuziki James Dandu ‘Mtoto wa Dandu’ kwa njia za kichawi.
Mara baada ya gazeti la Amani toleo namba 782 la Oktoba 17, mwaka huu kuripoti habari hiyo, mama Kanumba alipelekewa nakala yake nyumbani ambapo baada ya kuisoma, ndipo alipoona kuna kila sababu ya mchungaji huyo kukamatwa kwa kuwa atakuwa amehusika moja kwa moja na kifo cha mwanaye Kanumba. “Mama Kanumba alipata mshtuko mkubwa siku ile alipoliona lile gazeti, maskini alikuwa tayari ameanza kusahau machungu ya kuondokewa na mwanaye,” kilisema chanzo kilicho karibu na mama Kanumba.
Mama mzazi wa Kanumba, Flora Mtegoa.
Mara baada ya chanzo hicho kupenyeza habari hizo, paparazi wetu alimtafuta mama Kanumba ili kumuuliza alipokeaje habari za mchungaji huyo ambapo alipopatikana, alitiririka; “Naiomba serikali imkamate huyo mchungaji, maana yeye si amesema amemuua mwanangu, sasa iweje aendelee kutanua mtaani wakati ameweka wazi kuwa amemuua mwanangu. “Imeniuma sana, ameamsha machungu ambayo tayari nilianza kuyasahau. Huyo mchungaji akamatwe na sheria imchukulie hatua stahiki,” alisema mama Kanumba.
 
Marehemu Steven Kanumba.
Hata hivyo, katika ushuhuda alioutoa mchungaji huyo, alijitabiria kuwa ipo siku atakamatwa na kufungwa kutokana na siri za vigogo ambao aliwapa utajiri kwa nguvu za giza. “Nina siri za watu wengi sana, nikiwaambia mtaogopa na nchi itatikisika. Najua siku moja watu watanikamata na kunifunga pingu kwa siri nilizonazo, lakini kamwe siogopi kwa kuwa Bwana ameniongoza,” alisema.
Juzi gazeti hili lilifanya jitihada za kumtafuta mama Sharo Milionea, Zainabu Mkiete lakini hakupatikana kwani simu yake iliita bila ya kupokelewa. Mchungaji huyo alipotafutwa naye simu yake iliita bila kupokelewa.

SOMA HABARI YA MCHUNGAJI ALIYEDAI KUWAUA SHARO, KANUMBA: HAPA

No comments:

Post a Comment