JINA la Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, limeanza kutumiwa na baadhi ya
makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukusanya na kugawa fedha kwa kile
kinachoitwa “mbio wa kusaka urais.”
Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinasema kuwa wajumbe hao wamesema
mbio za Pinda kusaka urais zimekuwa na kishindo kikuu kwa sababu ya sera
yao kwamba “pesa itaongea.”
Baadhi yao wamefika mahali pa kumtambia Mbunge wa Monduli, Edward
Lowassa, ambaye naye anatajwa kuwania urais, huku mmoja wa wapambe wake
akisema, “Walidhani wao ndio wana pesa tu. Sasa tutawaonyesha kazi.”
Tanzania Daima lina taarifa kwamba Pinda ndiye tishio jipya la Lowassa,
na katika hatua ya kwanza ameshauriwa atumie fedha ya kutosha kufikia
wajumbe wengi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi,
wanaojulikana kama Wanec.
Inafahamika kwamba, kwa muda mrefu, Lowassa ndiye amekuwa na nguvu kubwa miongoni kwa wanec wa mikoa mingi.
Ili kukabiliana na nguvu hiyo, timu ya Pinda inadaiwa kuteua familia
moja yenye madaraka makubwa ya kisiasa jijini Dar es Salaam, kushika
mikoba yake. Taarifa zinasema mume akipita huku, mke anapita kule.
“Kazi ya kwanza waliyo nayo ni kulainisha wanec ambao ndio wapiga kura
za maoni watarajiwa. Lengo ni kuvuta kasi ya waliomtangulia, ambao
walishakuwa na mitandao imara ya wafuasi ndani ya NEC,” anadai mnec
mmoja ambaye anadai kushuhudia matukio kadhaa ya makundi ya watu kupewa
fedha kwa jina la Pinda.
Habari za ndani zinasema mtandao huo unafadhiliwa na matajiri na
wawekezaji kadhaa wanaowekeza katika maeneo nyeti, akisaidiwa na baadhi
ya watendaji wa serikali katika wizara nyeti ambayo imekuwa na migogoro
mingi kwa miaka tisa mfululizo. Wanakusanya fedha kutoka kwa matajiri
hao.
Baadhi ya wawekezaji wanaofahamika hadi sasa ni waziri mmoja mwenye
makeke na majivuno na katibu wake mkuu, ambao wanadiwa kukusanya fedha
kutoka kwa wawekezaji wa rasilimali za nchi ambazo zimekuwa zinaleta
mvutano na utata kati ya serikali na wananchi, kiasi cha kuchafua hali
ya kisiasa katika mikoa kadhaa ya Kusini mwa Tanzania.
Yumo pia tajiri mmoja anayemiliki mabasi, mbunge mmoja wa Zanzibar na
mzazi wa mbunge mmoja mwenye asili ya Kiasia, ambao wote kwa pamoja ni
wawekezaji katika biashara ya sukari.
Zipo taarifa kuwa mkubwa wanayempigania amesaidia kurahisisha wapate
vibali ya kuingiza sukari kwa wingi. Wamo pia wamiliki wa super market
moja maarufu ambayo imekuwa na utata katika miezi ya karibuni.
Ili kuwasilisha fedha hizo kwa wahusika, zinatumika fursa, sehemu na staili mbalimbali katika kugawiana pesa.
Miongoni mwa matukio makubwa yanayotajwa yanayohusisha wapambe na wanec hao ni haya yafuatayo:
Tarehe 20 Oktoba 2014, katika jengo moja la kisasa, jijini Dar es
Salaam, jirani na Hospitali moja maarufu yenye kutafiti na kuibu
magonjwa sugu nchini, mke wa mshika mikoba alikodi ofisi ambayo
aliitumia kukutana na wanec kadhaa na kuwagawia fedha.
Miongoni mwao ni wanec kutoka Kigoma Vijijini, Shinyanga na Bungeni,
ambao kila mmoja walipewa dola za Kimarekani 600, sawa na sh. milioni
moja ya Kitanzania.
Majina ya wanec hao tunayahifadhi kwa sasa. Tarehe hiyo hiyo, vijana
kadhaa wa UVCCM kutoka Ilala, nao walikutana na mshika mikoba huyo,
akawagawia sh. 200,000 kila mmoja.
Tarehe 16 Oktoba 2014, katika majengo ya NHC Dodoma, nyumbani kwa mbuge
mmoja wa Viti Maalumu kutoka Singida, mke wa mshika mikoba huyo anadaiwa
kupokea sh. milioni 24 kutoka ofisi moja ya umma, iliyo chini ya mabosi
hao wa wizara waliotajwa. Inasemekana fedha hizo zililetwa kwa agizo la
katibu mkuu husika, baada ya fungu la awali walilokuwa wamesafiri nalo
kwenye mabegi kuisha.
Baada ya kupokelewa na mshika mikoba, alikabidhiwa mnec mmoja kutoka Mbozi, akazigawa kwa baadhi ya wanec kutoka Zanzibar.
Tarehe 14 Oktoba 2014, wapambe hao na mshika mikoba walikutana nyumbani
mwa kigogo mkubwa serikalini, Masaki, Dar es Salaam, wakawezesha wanec
kadhaa kutoka Dar es Salaam, Tanga, Pwani na Zanzibar, kiasi cha sh.
milioni moja kila mmoja.
Baadaye, katika hoteli moja maarufu nje kidogo ya mji wa Dodoma, na
nyingine maarufu katikati ya mji, katika siku ya kwanza ya kikao cha
NEC, wanec wapatao 42 wanadaiwa kupokea sh. 200,000 kila mmoja kutoka
kwa mshika mikoba huyo na mkewe.
Kati ya tarehe 15 hadi 18 Oktoba 2014, mshika mikoba huyo na mkewe
waligawa fedha kwa wanec kwa viwango vya sh.300,000; 500,000 na 700,000.
Makatibu wa Wilaya wanadaiwa kupewa sh.150,000 hadi 300,000.
Tarehe 18 Oktoba 2014, asubuhi kabla ya wajumbe kuondoka, wanec kadhaa
kutoka Mkoa wa Kagera wanadaiwa kupokea sh. milioni moja kila mtu.
Hali hii ndiyo ilimfanya Makamu Mwenyekiti wa CCM Phillip Mangula,
wakati anawasilisha taarifa ya kamati ya maadili kwenye NEC, akasema
kwamba amegundua kuwa pale Dodoma kumezuka ATM mpya. Alionya kuwa
wahusika wataitwa na kuonywa.
Kutokana na makeke ya wapambe hawa wanaotumia jina la Pindi kugawa
fedha, zipo taarifa kwamba tayari kamati ya maadili imemuita na kumuonya
waziri mkuu kuhusiana na tuhuma hizi.
Kauli za wahusika
Gazeti hili lilipomuuliza Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape
Nnauye, kuhusu ukweli wa taarifa hizo, alisema: “Mimi nazisikia kutoka
kwako, kama mmeziokota bafuni au chooni mtajua ninyi lakini mimi ndiyo
nazisikia kutoka kwako,”
Mnec kutoka Kigoma alipoulizwa kuhusu fedha hizo, alikanusha, lakini
alikiri kwamba juzi alikuwa katika jengo jirani na Hospitali ya Ocean
Road.
Alisema jengo lile ni la ofisi, na kwamba alienda katika moja ya ofisi
ya jengo hilo kwa shughuli zake binafsi. Alikana kukutana na mke wa
mshika mikoba huyo, lakini akasisitiza kuwa alikwenda pale kwa shughuli
zake binafsi.
Katika hatua ya kujichanganya, Mnec huyo aliuliza kama kuna taarifa
zozote zinazomuhusu. Alipoelezwa kuwa zipo bila kujua ni taarifa gani,
alianza kujitetea kuwa kwa nafasi yake, yeye ni mtu mdogo asiyeweza
kuhusishwa katika makundi ya wawania urais kupitia CCM.
“Mimi ni mtu mdogo sana tena mkulima wa mihogo kutoka Kigoma. Hayo
makundi ni ya watu wakubwa. Kwanza hata pombe sinywi sasa nitakaa nao
wapi?”alihoji.
Alipoulizwa sababu ya kujitetea kuwa hayupo katika makundi hayo ilihali
mwandishi hajamueleza kama habari aliyonayo inahusiana na makundi ya
urais, Mnec huyo aliomba kukutana na mwandishi katika hoteli ya Harare
Inn, Dar es Salaam, jambo ambalo halikutekelezwa na mwandishi.
Mnec mwingine atokaye Shinyanga, alipoulizwa kuhusu fedha alizopokea
juzi, alisema mwandishi amemfananisha na mtu mwingine, kwani yeye
hahusiki.
Alipoulizwa ataje mtu aliyefananishwa naye, aliomba mwandishi ampigie
simu baadaye kwa kuwa muda huo alikuwa katika mkutano. Jitihada za
gazeti hili kumpigia simu hazikuzaa matunda baada ya namba yake kuita
bila kupokewa na wakati mwingine simu ilikatwa.
Mnec wa Tabora alidai kwamba hajawahi kufika katika jengo hilo kwa ajili
ya kupokea fedha kutoka kwa mke wa mshika mikoba wa Pinda.
Alisema kuwa tangu alipopata ajali hajaweza kufanya shughuli yoyote hata
kuhudhuria vikao vya kamati ya bunge vilivyoanza juzi jijini Dar es
Salaam, na kwamba kwa muda huo alikuwa katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya.
“Ninyi si mnajua kuwa ninaumwa nilipata ajali ya gari hata gazeti lenu
liliandika ajali hiyo sasa iweje niende huko wakati sijaanza kutoka?
Lakini nikwambie wewe ni mtu wa pili kunipigia simu na kuniuliza swali
hilo wa kwanza ni kaka yangu Hussein nikamueleza kuwa sijaenda kuchukua
fedha kwa mtu yeyote yule,” alisema.
Mshika mikoba na mkewe simu zao hazikupatikana kabisa hewani kwa siku nzima ya jana.