Wednesday, 1 October 2014

NANI HAJAZOMEWA YANGA SC…SIMON MSUVA?



KOCHA Mbrazil, Marcio Maximo alimuanzisha kwa mara ya kwanza ya beki Edward Charles Yanga SC ikicheza na Prisons ya Mbeya katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. Alicheza kwa sababu beki chaguo la kwanza la timu hiyo, Oscar Joshua alikuwa majeruhi baada ya kuumia katika mchezo wa kwanza na Mtibwa Sugar mjini Morogoro. Yanga SC ilivutiwa na beki huyo akiichezea timu ya taifa, Taifa Stars kutoka JKT Ruvu na moja kwa moja ikaamua kumsajili. Wataalamu wengi wa soka nchini wamempaasisha beki huyo na kumtabiria atakuwa tegemeo la taifa muda si mrefu na anaweza kufika mbali pia akijibidiisha na akawa na malengo hayo pia.
Beki mpya wa Yanga SC, Edward Charles alikumbana na zomea zomea Jumapili timu hiyo ikicheza na Prisons
Yanga SC ni timu kubwa, mchezaji anahitaji muda kuzoea kuichezea na kuanza kufanya vizuri, vivyo hivyo kwa Edward Jumapili alianza vibaya dakika za mwanzoni. Alikuwa anaharibu hadi baadaye alipozoea hali na kuanza kucheza bila wasiwasi hata akawa miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri na kuchangia ushindi wa 2-1. Mashabiki wa Yanga SC huwa hawana subira, Charles alipoharibu mara mbili tatu, wakaanza kumzomea. Lakini kijana huyo alisimama imara na kuanza kucheza vizuri baadaye, akipanda kusaidia mashambulizi na kurudi kulinda vizuri. Edward Charles, beki mrefu mwenye hatua nzuri, ameonyesha dalili anaweza kuwa tegemeo la Yanga SC katika nafasi hiyo pamoja na Taifa Stars. Lakini lazima mashabiki wa Yanga SC wamvumilie, ili azoee hali taratibu na kucheza vizuri zaidi. Tabia ya kuzomea wachezaji wanapokosea si nzuri na umefika wakati mashabiki wa Yanga SC lazima wabadilike. Mashabiki wa Yanga SC wakati fulani walikuwa wanamzomea Nahodha wao, Nadir Haroub ‘Cannavaro’. Walimzomea hadi Simon Msuva wakati fulani, lakini kwa sasa ukitaja wachezaji watatu ‘roho za Yanga’, wawili hao lazima watakuwamo kwenye orodha.
Simon Msuva ni miongoni mwa wachezaji waliofuzu mtihani wa kuzomewa kabla ya kuwa shujaa wa timu hiyo kwa sasa
Hili linaweza kuwa fundisho kubwa kwa mashabiki wa Yanga SC, kwamba kuzomea wachezaji si desturi nzuri. Unajisikiaje, jana ulimzomea, leo unamshangilia Simon Msuva. Basi acha kuzomea wachezaji kuanzia sasa. 

No comments:

Post a Comment