Tuesday, 14 October 2014

PISTORIUS AOMBEWA KIFUNGO CHA NYUMBANI




Oscar Pistorius
Idara ya kurekebisha tabia nchini Afrika Kusini inataka Oscar Pistorius apewe kifungo cha nyumbani cha miaka mitatu kwa kumpiga risasi na kumuua mpenziwe Reeva Steenkamp.

Bwana Joel Maringa afisa anayehusika na masuala ya urekebishaji tabia aliiambia mahakama mjini Pretoria kuwa hawamuadhibu tu Pistoruiis bali pia wanataka kumbadili kitabia akisema kuwa anaweza kutoa huduma za jamii kwa saa 16 kwa mwezi.

Awali daktari wa Pistorius anayehusika na matatizo ya akili Lore Hartzenberg aliiambia mahakama kuwa mwanariadha huyo mlemavu amevunjika moyo baada ya kumuua mpenziwe.

Shahidi wa tatu ambaye ni meneja wa shirika la Pistorius la Peet Van Zyl aliiambia mahakama kuhusu orodha ya huduma zake zikiwemo za shirika la kuwahudumia watoto la Umoja wa Mataifa kama balozi mwema. Kesi hiyo inatarajiwa kuchukua muda wa siku tatu.

Kwa upande wake mwendesha mashitaka Gerrie Nel ameelezea pendekezo hilo la Bwana Maringa kuwa "linashtua na si sahihi"akisema zaidi kuwa ingekuwa bora kusiwe na adhabu kabisa, huku akihoji kama Bwana Maringa alijua ukubwa wa kosa la Pistorius.

Baba wa Bi Steenkamp, Barry, alishika kichwa wakati Bwana Maringa akizungumza, huku marafiki wa marehemu wakitikisa vichwa kwa mshangao wa kile kilichoelezwa na Bwana Maringa.

Pistorius alipatikana na hatia ya kumuua Bi Steenkamp bila kukusudia mwezi uliopita -lakini aliondolewa mashitaka ya kuua.

Uamuzi huo ulishutumiwa na ndugu wa familia ya marehemu.

Pistorius anakabiliwa na kifungo cha miaka 15 jela, japokuwa Jaji Thokozile Masipa anaweza kuondoa kifungo hicho au kumtoza faini.


Amesema mwanariadha huyo alifanya "uzembe" wakati alipompiga risasi mpenzi wake kupitia mlango wa choo, akidhani ni mhalifu kutoka nje.

No comments:

Post a Comment