Mnamo tarehe 18 Oktoba 2014, Wizara ilipokea taarifa kutoka Ofisi ya
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ya kuwepo kwa mgonjwa aliyehisiwa kuwa na
ugonjwa wa Ebola. Mgonjwa huyu aliyekuwa na umri wa miaka 17, jinsia ya
Kike na mkazi wa kijiji cha Bupandwa Tarafa ya Kahunda Wilaya ya
Sengerema, alilazwa akiwa na dalili za homa kali, manjano, kutokwa na
damu sehemu mbalimbali za mwili.
Hata hivyo, mgonjwa huyu hakuwa na historia ya kusafiri kwenda nchi
zilizoathirika na ugonjwa wa Ebola na hakuwahi kupokea mgeni kutoka nchi
hizo ndani ya siku ya 21 zilizopita.
Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na;
i.Sampuli ya damu ya mgonjwa kwa ajili ya uchunguzi wa Kimaabara
ilipokelewa tarehe 18 Oktoba, 2014. Matokeo ya awali dhidi ya magonjwa
ya jamii ya ebola yakiwa ni pamoja na Dengue na Chikungunya yanaonyesha
kuwa mgonjwa hakuwa na magonjwa haya. Uchunguzi wa kimaabara bado
unaendelea na Wizara itatoa taarifa rasmi pindi utakapokamilika.
ii.Mgonjwa alihudumiwa katika chumba maalumu kilichotengwa ambapo
wahudumu pamoja na walioshughulikia mazishi yake walivaa vifaa kinga
(PPE)
iii.Wataalamu pamoja na ndugu waliomhudumia mgonjwa kabla ya mauti kumfika wametengwa na wapo kwenye uangalizi maalumu
Mwongozo wa utambuzi wa ugonjwa huu (Standard Case Definition)
unaeleza kwamba ili mgonjwa aweze kuhusiwa kuwa na ugonjwa wa Ebola
anatakiwa akidhi vigezo ifuatavyo:
i. Dalili za awali ni homa kali ya ghafla, kulegea mwili, maumivu ya
misuli, kuumwa na kichwa, na kutokwa na vidonda kooni. Mara nyingi
dalili hizi hufuatiwa na kutapika, kuharisha,kutokwa na vipele vya
ngozi, kwa baadhi ya wagonjwa hutokwa na damu ndani na nje ya mwili
ii.Awe amesafiri kwenda sehemu zilizothibitishwa kuwa na ugonjwa wa ebola ndani ya kipindi cha wiki 3
iii. Kugusa majimaji kutoka kwa mgonjwa, maiti au mnyama anayehisiwa au kuthibitishwa kuwa na ugonjwa wa Ebola.
HitimishoWizara inapenda kuwatoa hofu wananchi kuwa hadi sasa HAKUNA
MGONJWA yeyote aliyethibitishwa kuwa na virusi vya ugonjwa wa Ebola hapa
nchini. Hata hivyo uchunguzi wa kina wa Kimaabara unaendelea na taarifa
itatolewa baada ya majibu kupatikana.
No comments:
Post a Comment