Tuesday 3 December 2013

Toure ndiye bora zaidi Afrika

by zangii ze icon
Yaya Toure aliteuliwa mara tano kuwania tuzo hili lakini akafanikiwa kushinda mwaka huu
Yaya Toure ametangazwa mshindi wa tuzo ya BBC ya mwaka 2013 ya mchezaji bora zaidi wa soka barani Afrika.
Mchezaji huyo wa Ivory Coast, na ambaye pia ni kiungo wa klabu ya Manchester City ya Uingereza, na ambaye jina lake limekuwepo kwa miaka minne iliyopita katika orodha ya wachezaji wanaowania tuzo, aliwashinda Pierre-Emerick Aubameyang, Victor Moses, John Mikel Obi na Jonathan Pitroipa, katika kuibuka mshindi.
Mchezaji huyo ana umri wa miaka 30.
Orodha fupi ya waliowania tuzo hiyo ilitayarishwa na wataalamu 44 wa soka kutoka kote barani Afrika, na wakizingatia hasa maarifa ya mchezaji, kiufundi, ushirikiano na wenzake katika timu, na kwa kucheza mchezo safi na kwa haki.
Kisha, kupitia idadi kubwa kabisa kuandikishwa kwa wapiga kura, mashabiki waliweza kushiriki katika shughuli hiyo katika mtandao, au kupitia ujumbe wa simu ya mkononi.
Mashabiki hao wameamua kwamba Toure ndiye bora zaidi, kwani katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, raia huyo wa Ivory Coast alicheza kwa bidii, kuonyesha mchezo wa kasi, ubunifu, na vile vile kwa kufunga magoli.
Ingawa mwaka 2013 ulikuwa ni wa ufanisi kwa Toure hasa kwa kupata vikombe, hakuweza kuisaidia nchi yake, wala klabu, kupata kombe lolote lile, lakini bado alionyesha kiwango cha hali ya juu katika mchezo.
Baada ya kuvunjika moyo kwa kushindwa kuutetea ubingwa wao wa ligi kuu ya Premier wa mwaka 2012 akiichezea Manchester City, Toure alirudi uwanjani akijizatiti, na kuimarisha mikwaju yake ya free-kick.
Alitumbukiza wavuni bao, kwa mpira wa kupinda, katika siku ya kwanza ya msimu mpya wa ligi kuu ya Premier, wakati timu yake ilipocheza na Newcastle, na akarudia hayo hayo katika mechi iliyofuata wakati Hull walipowatembelea katika uwanja wao wa nyumbani.
Toure amefunga magoli manne ya kupanga kwa makini shambulio, na hayo yakiwa ni kati ya magoli saba kwa jumla aliyoweza kuifungia klabu ya Man City msimu huu.
Kufikia sasa, mwaka huu wa 2013, Toure ametumbukiza wavuni jumla ya magoli 12; ya klabu na vile vile ya nchi yake, na hiyo ni rekodi nzuri sana kwa mchezaji wa kiungo cha kati.
Mbali na ustadi huo katika kumalizia, Toure ni kiongozi bora katika timu, na maarifa yake yameiwezesha City kufikia sasa kuwa katika nafasi ya nne katika ligi kuu ya England.
Aliisaidia kikamilifu nchi yake ya Ivory Coast kufuzu kwa michuano ya Kombe la Dunia ya mwaka ujao itakayofanyika nchini Brazil.
Timu yake ya Tembo, The Elephants ilihitaji kuusahau mwanzo mbovu hapo awali katika kampeni yao ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, na walipoondolewa katika robo fainali na Nigeria, ambao hatimaye waliibuka mabingwa, na Toure akiwapa matumaini ya kufanya vyema baadaye.
Nje ya uwanja, Toure ameongoza vita dhidi ya ubaguzi wa rangi katika soka, hasa baada ya matusi kuelekezwa kwake katika mechi ya ligi ya klabu bingwa dhidi ya CSKA Moscow, mwezi Oktoba, na akionyesha moyo wa uvumilivu na wa kimichezo unaostahili uwanjani.
Tukio kama hilo linaweza kumvunja moyo mchezaji asiyejiamini, lakini Toure ameendelea kuwa mchezaji wa kipekee tangu wakati huo.
Na katika mwaka wa tano baada ya jina lake kupangwa katika orodha ya wachezaji wanaowania tuzo, hatimaye Toure ametajwa kama mshindi wa tuzo ya mchezaji bora zaidi wa soka barani Afrika.

No comments:

Post a Comment