BY ZANGII ZE ICON
KATIKA hali ya kushangaza, siku chache baada ya kuripotiwa kupona na kuacha matumizi ya madawa ya kulevya, mwanamuziki Rehema Chalamila ‘Ray C’ anadaiwa kugeuka mwanamasumbwi na kumpa kipigo mwigizaji Nuru Nassoro ‘Nora’,.
Kwa mujibu wa shuhuda wetu, tukio hilo lilijiri wiki iliyopita ndani ya studio moja ya kurekodia muziki iliyopo Kinondoni, Dar ambapo wawili hao walikutana walipokwenda kurekodi ngoma zao.
Ilidaiwa kuwa akiwa studio hapo, Nora alikutana na Ray C ambaye pia alizama mahali hapo bila mawasiliano na prodyuza anayemtengenezea ngoma mpya.
Chanzo hicho kilipasha kuwa baada ya Ray C kuingia studio hapo alimkuta prodyuza huyo akiandaa ngoma ya Nora ambapo alihoji kilichompeleka mwigizaji huyo mahali hapo.
Ilidaiwa kuwa prodyuza huyo ambaye jina halikupatikana alimwambia Ray C kuwa Nora alifika kurekodi wimbo wake.
Ilisemekana kuwa Ray C hakuridhishwa na majibu hayo, akaomba asikilizishwe ngoma hiyo ya Nora lakini baada ya kusikiliza ilidaiwa kwamba Ray C aliiponda mbele ya Nora, jambo ambalo mwigizaji huyo hakufurahishwa nalo.
Ilidaiwa kuwa Nora alipandwa hasira na kujikuta akimjibu mbovu Ray C.
Habari ziliendelea kutiririka kuwa siku hiyo walimalizana kwa kusonyana na siku iliyofuta walikutana tena studio hapo ambapo Ray C alidaiwa kutinga akiwa ‘masanga’.
Ilisemekana kuwa alipomuona Nora alianza kumpa vijembe, jambo lililosababisha Nora kushikwa hasira ndipo wakavaana na kuzichapa.
Hata hivyo, ilidaiwa kuwa Ray C ndiye aliyeibuka bingwa wa ndondi hizo kwa kumtwanga Nora hadi kumvimbisha jicho kabla ya maprodyuza na watu wengine kufanya kazi ya ziada kuwaamulia.
Ilisemekana kuwa baadaye Ray C alitolewa nje ndipo akahamishia hasira kwenye gari la Nora aina ya Toyota Vitz kisha akalivunja kioo na kutambaa zake.
Baada ya kupenyezewa ‘niuz’ hizo tulimtafuta Nora ambaye alikiri kutokea kwa sekeseke hilo huku akibainisha namna alivyoumizwa jicho lake na kuvunjiwa kioo cha pembeni cha gari lake.
Aliongeza kuwa siku hiyo alipoteza pochi wakati wa ugovi huo.
“Ray C alinikuta studio nikifanya wimbo, kilichonishangaza baada ya kuniona tu alibadilika ghafla.
“Nilijua angenishauri kwa kuwa ndiyo ninaanza gemu kumbe mwenzangu alifikiria vingine,” alisema Nora na kuongeza:
“Mbali na kuniumiza jicho lakini alinifanyia mambo ya ajabu sana, kama kusingekuwa na watu wa kutuamulia basi chochote kingetokea.
“Sikwenda kuripoti polisi. Niliamua kusamehe kwa sababu kuna watu walinisihi niachane naye kwa sababu bado kuna mambo yanamwendesha.
Kwa upande wake Ray C alitafutwa kwa kila njia kupitia simu ya mkononi na kumvizia studio lakini hakupatikana hivyo juhudi za kumpata zinaendelea.