Tuesday 15 October 2013

Julio amchongea Minziro Yanga

by rahim kassonga

VIJEMBE ni jambo la kawaida Ulaya hasa inapofika kwenye mechi kubwa.
Hali hiyo nayo ipo Bongo kwa Simba na Yanga wakati huu timu hizo zikijiandaa na pambano lao la Jumapili ijayo la Ligi Kuu Bara.
Sikia hii. Kocha Msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ amekumbushia kichapo cha mabao 3-0 ambacho Yanga walikipata kutoka kwa Mtibwa Sugar msimu uliopita.
Julio alidai alipokuwa anaifundisha timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 20 wakiwa kambini mjini Mbeya, usiku alikutana na wachezaji wa Yanga, Mnyarwanda Haruna Niyonzima ‘Fabregas’ na Athuman Idd ‘Chuji’ wakiwa baa, huku kocha wao msaidizi, Fred Minziro akishuhudia.
Julio alisema tukio hilo lilitokea baada ya Yanga kucheza na Prisons na kutoka suluhu na yeye kwa sababu alichukizwa na kitendo kile aliwasema wazi bila kuogopa.
“Kitendo kile kiliniuma, niliwaona wachezaji wale na baadhi yao ni Chuji na Niyonzima wakati walikuwa wanajua wana mechi na Mtibwa Sugar, nikiwa kama kocha wa timu ya taifa niliwasema kwa sababu iliniuma na kama nadanganya, muulizeni mwandishi huyu hapa alikuwepo (anamnyooshea kidole) akatae,” alisema Julio katika mkutano na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki.
Hata hivyo, Minziro amejibu mashambulizi kwa Julio na kumwambia: “Kama yeye amemwaga mboga, mimi nitamwaga ugali kwa nini azungumze mambo ya mwaka jana ambayo si ya kweli.”
Minziro alienda mbali na kusema, sababu ya Julio kuongea mambo hayo ni hofu ya kipigo cha Jumapili na anatafuta sababu ya kuwaharibia watu majina.
“Ishu hiyo ya Mbeya, nilienda kumfuata mwanangu na ndipo nilipomkuta Julio na wachezaji na si kwamba alinikuta mimi na wachezaji,” alifafanua bila kuingia kiundani.
source:mwanaspoti

No comments:

Post a Comment