Monday, 7 October 2013

SHAHIDI KATIKA KESI YA RUSHWA MTWARA AHUKUMUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA MIWILI JELA KWA KUSEMA UONGO MAHAKAMANI



Bw. ISSA BAKARI MATWANI Katibu wa CCM Tawi la Naulongo Kata ya Naliendele Manispaa ya Mtwara, Mkoani Mtwara, amehukumiwa kifungo cha miaka 2 gerezani au kulipa faini la shilingi laki moja kufuatia Mahakama kubaini kuwa kwa makusudi alikana maelezo aliyokuwa ameyatoa TAKUKURU katika shauri la Rushwa kwenye uchaguzi wa Diwani mwaka 2010.
Bwana ISSA BAKARI MATWANI alikuwa shahidi muhimu kwenye shauri la Na. 85/2011 kati ya Jamhuri dhidi ya SALMA HAMIS CHITOPE ambapo akiwa Katibu wa CCM Tawi la Naulongo Kata ya Naliendele Mtwara mnamo mwezi Mei, 2010 aliandaa orodha ya majina ya mgao wa Rushwa kwa ajili ya mgombea kiti cha Udiwani Kata ya Naliendele Bi. SALMA HAMIS CHITOPE ambaye aliibuka mshindi
Awali Bw. ISSA BAKARI MATWANI aliandikisha maelezo yake TAKUKURU na kukiri kuandaa orodha hiyo ya mgao wa Rushwa kwa wapiga kura na hivyo kufanywa shahidi muhimu katika shauri hilo -baada ya Mtuhumiwa Bi SALMA HAMIS CHITOPE kukamatwa akiwa na orodha ya majina ya mgao wa Rushwa kabla ya kufikishwa Mahakamani
Katika hali isiyo ya kawaida, akiwa anatoa ushahidi Mahakamani mnamo 23/5/2012 Bw. ISSA BAKARI MATWANI mbele ya Hakimu Mkazi Mheshimiwa Ernest Mbungu, alikana maelezo yote aliyoyatoa kwa Maafisa wa
TAKUKURU wakati wa uchunguzi ; hivyo kuifanya Mahakama kukosa nafasi ya kutathmini ushahidi wake.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Sospeter S. Tyeah uliiomba Mahakama imwone shahidi kama aliyegeuka Mahakamani (hostile) ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake. Hatimaye, baada ya Mahakama kuridhika na mazingira ya ushahidi huo ilikubaliana na upande wa mashtaka na kumtangaza ISSA BAKARI MATWANI kuwa ni shahidi kigeugeu (hostile)
Kufuatia hatua hiyo ya Mahakama, Jamhuri ilifungua shauri Na 135/2012 dhidi ya BAKARI ISSA MATWANI katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara 5/9/2012 kwa kosa la kutoa maelezo ya uongo (perjury) kwa Afisa Uchunguzi wa TAKUKURU akiwa chini ya kiapo.
Shauri hili ambalo lilivuta hisia za wakazi wengi wa Manispaa ya Mtwara na wanachama wa CCM na vyama vingine, lilifikia tamati hivi karibuni ambapo Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mtwara, Mheshimiwa Joseph Fovo alimtia hatiani Bw. ISSA B. MATWANI kwa kosa la kutoa ushahidi wa uongo Mahakamani huku akizuia Mahakama kutenda haki katika shauri ambalo TAKUKURU kwa niaba ya Jamhuri ilikuwa ikimshtaki Diwani SALMA HAMIS CHITOPE.
Baada ya kumkuta ana hatia, Mahakama ilimhukumu Bw. ISSA BAKARI MATWANI kwenda jela miaka miwili ama kulipa faini ya Tshs. 100,000/= (Laki moja tu) ili iwe fundisho kwa wote wanotoa maelezo ya uongo wakiwa chini ya kiapo na kuidanganya Mahakama katika ushahidi wanao ufahamu.
IMETOLEWA na:-
AIDAN A. NDOMBA
MKUU WA TAKUKURU (M)
MTWARA.................................06.09.2013

No comments:

Post a Comment