Wednesday, 23 October 2013

SERIKALI YA TANZANIA YASEMA MIKATABA YA USHIRIKIANO BAINA YA RWANDA, KENYA NA UGANDA SIO HALALI

by rahim kassonga (La Captain)

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza kuwa mikataba ya ushirikiano iliyotiwa saini hivi karibuni baina ya Rwanda, Kenya na Uganda sio halali kwani makubaliano hayo yanapaswa kupitia mfumo wa sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki {EAC}.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kutoka Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Bi Vedastina Justinian ambaye amesisitiza kwamba mikataba iliyotiwa saini na Rwanda, Kenya na Uganda bila ya kuzishirikisha Tanzania na Burundi si halali na kwamba, ni kinyume na utaratibu wa jumuiya hiyo.
Justinian ameongeza kuwa mikataba ya Marais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Paul Kagame wa Rwanda na Yoweri Museveni wa Uganda inapaswa kuidhinishwa kwanza na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na tayari serikali ya Tanzania imeuandikia rasmi uongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ikihoji kuibuka kwa utaratibu wa baadhi ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo kujadili masuala ya utangamano bila ya kuishirikisha Tanzania.
SOURCE:DAWATI
EDITOR:IRENE TEMU

No comments:

Post a Comment