Thursday 21 November 2013

UNESCO YAITAKA SERIKALI KUZITAMBUA REDIO ZA JAMII NCHINI

DSC05297
Mgeni rasmi Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Assah Mwambene (kushoto) akiwasili katika Hoteli ya New Palm Tree iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani kufungua mkutano wa nne wa Mtandao wa vyombo vya habari vya Kijamii nchini (COMNETA) akiwa ameongozana na wenyeji wake Afisa Mipango Taifa wa Kitengo cha Mawasiliano na Habari na mratibu wa miradi ya UNESCO , Yusuph Al-Amin (wa pili kulia), Mwenyekiti wa COMNETA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Redio ya Jamii ya Wilayani Karagwe ya FADECO Bw.Joseph Sekiku (wa pili kushoto) na Makamu Mwenyekiti wa COMNETA ambaye pia ni Meneja wa Kituo cha Habari na Mawasiliano cha Telecentre Sengerema FM mkoani Mwanza Bw. Felician Ncheye.
Na.Mwandishi wetu
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni,(UNESCO), limeiomba Serikali kutambua mchango wa redio za jamii katika maendeleo nchini na hivyo kufanya nao kazi kwa karibu.
Ombi hilo limetolewa jana na Afisa Mipango Taifa wa Kitengo cha Mawasiliano na Habari na mratibu wa miradi ya UNESCO , Yusuph Al-Amin wakati wa mkutano wa Mtandao wa vyombo vya habari vya Kijamii nchini (Community Media Network of Tanzania – COMNETA)unaofanyika mjini Bagamoyo.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Al-Amin aliwapongeza COMNETA kwa kufanikiwa kuanzisha umoja huo ambao awali kulikuwa na vituo viwili tu vilivyokuwa vikitambuliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), huku kwa sasa vikifikia vituo zaidi ya 27, kwa nchi nzima ikiwemo Tanzania Bara na Visiwani.
DSC05299
Mgeni rasmi Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Assah Mwambene akibadilishana mawazo na wenyeji wake kabla ya kufungua mkutano wa nne wa COMNETA unaoendelea Bagamoyo mkoa wa Pwani.
Akifafanua zaidi, Al-Amin alisema UNESCO imekuwa ukiisaidia COMNETA kufikia malengo yake kwa kutambua kuwa radio hizo zinafanya kazi katika jamii na zina uwezo mkubwa wa kuifikia jamii inayoizunguka.
“Zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania wako vijijini na hawa wanafikiwa kwa karibu zaidi na radio jamii, kwa kupata taarifa za kina na za haraka” alisema Al-Amin.
Alitoa mfano wa Radio ya jamii iliyoko Micheweni, Pemba ambayo uwepo wake umesaidia sana kuleta mabadiliko ya maendeleo wilayani hapo tofauti na ilivyokuwa huko nyuma ambapo wilaya hiyo likuwa nyuma sana kimaendeleo.
‘Vipindi mbalimbali vya kuhamasisha maendeleo vinavyorushwa na redio hii vimesaidia sana kuhamasisha wananchi na sasa mwamko wa maendeleo umekuwa mkubwa hapo Micheweni” alisema, Al-Amin.
DSC05318
Mwenyekiti wa COMNETA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Redio ya Jamii ya Wilayani Karagwe ya FADECO Bw.Joseph Sekiku akizungumza na WanaCOMNETA kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Assah Mwambene.
Aliwashauri wanachama wa COMNETA, wawe na umoja, mshikamano na kupendana ili kuepuka migogoro inayoweza kuyumbisha ustawi wa chama. “Tunawaomba sana, COMNETA, muwe mfano wa kuigwa kwa kuepuka migongano ya wenyewe kwa wenyewe ikiwamo kugombea madaraka ili kuwa umoja wa mfano kwa katika tasnia ya vyombo vya habari hapa nchini’.
Kwa upande wake, mgeni rasmi katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Assah Mwambene aliupongeza umoja huo na kuwataka kuendelea kuwa daraja muhimu la kuipasha jamii mambo yote ya msingi bila kuvunja misingi ya kitaifa ikiwemo kulinda maslahi ya taifa.
“Kwanza kabisa, niwapongeze, COMNETA kwa kuanzisha umoja wenu huu, na kuwapo kwangu hapa leo kunanifunza mengi, hivyo kwa yale yote mulioniomba nami, nitayafikisha kwa wahusika na kuyafanyia kazi” alisema, Mwambene.
Aidha, akijibu maswali mbali mbali ya wajumbe yaliyokuwa yakitolewa kwenye mkutano huo, Mwambene aliwahakikishia kuwa Serikali inatambua mchango wa vyombo vya habari na inatarajia kupeleka muswada wa sheria ya vyombo vya habari kwenye Bunge lijalo.
“Muswada wa habari upo tayari, tunatarajia utapelekwa Bungeni katika kikao kijacho mwezi Desemba ili kujadiliwa.Tunaamini Kamati husika ya Bunge itawakaribisha wadau wa tasnia ya habari ili kutoa mawazo yao katika muswada huo kabla haujafikishwa bungeni,” alisema.
DSC05335
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Assah Mwambene akitoa risala wakati akifungua mkutano wa siku nne wa COMNETA unaoendelea mjini Bagamoyo mkoa wa Pwani.
DSC05357

Akidokeza juu ya yaliyomo ndani ya muswada huo, Mwambene alisema umebainisha wazi ulazima wa wamiliki wa vyombo vya habari kuwakatia bima za afya na usalama kazini waajiriwa wao pamoja na suala la maslahi stahiki kwa waandishi wa habari. Muswada huo pia umependekeza kiwango cha elimu kwa mwandishi wa habari kiwe shahada ya kwanza.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa COMNETA, Bw. Felician Nchewe aliomba Serikali ivifikirie vyombo vya Jamii nchini, katika kufikia malengo yake.
DSC05408
Afisa Mipango Taifa wa Kitengo cha Mawasiliano na Habari na mratibu wa miradi ya UNESCO, Bw.Yusuph Al-Amin akizungumza mbele ya mgeni rasmi Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) wakati wa ufunguzi wa mkutano wa nne wa WanaCOMNETA uliofunguliwa rasmi jana wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani.
“Kwa sasa COMNETA, tumefikia malengo mbali mbali, hivyo tunaiomba sana Serikali ivifikie vyombo hivi vya Jamii, kama ilivyo kwa wenzetu kupitia TCRA, kuvisaidia vituo vya Tele Centre kufikia malengo yao” alisema Nchewe.
Kwa upande wake, Mkufunzi wa radio za Jamii kutoka UNESCO, Mama Rose Hajj Mwalimu alisema mkutano huo wa COMNETA wa siku nne, ni wa kuweka mifumo na mikakati bora ya uendashaji wa vituo hivyo na kuweka maazimio ya kufanyia kazi. Ambapo uliwahusisha Mameneja na Wakurugenzi kutoka radio za Jamii (Community Radio) zilizopo nchini.
Mkutano huo unaendelea katika hoteli ya New Palm Tree Village, Bagamoyo.
DSC05371
Meneja wa Redio Kahama FM Marco Mipawa akichangia maoni yake juu ya sheria ya Magereza wakati wa mkutano wa nne wa COMNETA unaohusisha redio za Jamii nchini uliofadhiliwa na Shirika la UNESCO kupitia mradi wa DEP.
DSC05384
Afisa Habari wa Kitengo cha Habari cha Umoja wa Mataifa (UNIC) Bi. Usia Nkhoma Ledama akitoa maoni yake katika mkutano huo
DSC05303
Baadhi ya washiriki wakisikiliza mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa wakati wa mkutano wa nne wa COMNETA unaoendelea Bagamoyo mkoani Pwani.
DSC05272
Erick Kalunga kutoka Ubalozi wa Uswiss ambao wanadhamini mradi wa SIDA akizungumzia furaha yao kuona miradi wanayofadhili inapiga hatua na kuleta maendeleo kwa jamii.
DSC05432
Mwenyekiti wa Tanzania Telecentre Network (TTN) Bw. Hirnoy Barmeda akizungumzia umuhimu wa Telecentre kwa jamii.
DSC05441
Mkurugenzi wa taasisi isiyo ya kiserikali ya Barmedas na Jamii Foundation Crystal Kigoni akifafanua kuhusu taasisi yao isiyo ya Kiserikali inayojishughulisha na mambo ya ustawi wa Jamiikupitia vyombo vya habari na Teknohama kwa kuibua mambo yanayotokea mitaani kwa jamii inayozunguka Redio za Jamii.
DSC05446
Washiriki wa mkutano wa nne wa COMNETA unaoendelea wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
DSC05453
Mkutano wa nne wa WanaCOMNETA ukiendelea katika hoteli ya New Palm Tree wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani.
DSC05450
Mratibu wa Mtandao wa Jinsia na Habari Tawi la Tanzania (GEMSAT) Bi. Gladness Hemedi Munuo akiongelea usawa wa jinsia katika Uongozi na Utawala kwa Redio za Jamii.
IMG_4988
Mshauri wa UNESCO, Balozi mstaafu Mh. Celestine Liundi akisisitiza umuhimu wa kuhubiri amani kwa redio za Jamii nchini.
DSC05265
Meneja wa mradi wa DEP kutoka UNESCO Courtney Ivins akibadilishana mawazo na Mwenyekiti wa COMNETA ambaye pia ni Mkurugenzi wa Redio ya Jamii ya Wilayani Karagwe ya FADECO Bw.Joseph Sekiku kwenye mkutano wa WanaCOMNETA unaoendelea wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani.
DSC05422
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bw. Assah Mwambene katika picha ya pamoja na WanaCOMNETA mara baada ya kufungua mkutano wa nne wa COMNETA wilayani Bagamoyo.
DSC05425
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Assah Mwambene katika picha ya pamoja na Bodi ya COMNETA.
DSC05420
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Assah Mwambene (kulia) akibadilishana mawazo na Mshauri wa UNESCO, Balozi mstaafu Celestine Liundi (katikati) pamoja Mkufunzi wa Mafunzo hayo ambaye pia ni Mjumbe ya wadhamini COMNETA Bw. Gervas Mushiro (kushoto)

No comments:

Post a Comment