Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) limetangaza maandamano kwenda Ikulu kumuomba Rais Jakaya Kikwete asikubali kutia saini Rasimu ya Katiba inayopendekezwa iwapo itapitishwa na Bunge.
Mwenyekiti wa Bawacha, Halima Mdee alisema jana kwamba maandamano hayo yatafanyika mwishoni mwa wiki ijayo, baada ya maandalizi yatakayofanyika kwa siku saba kuanzia jana kukamilika.
Mdee ambaye pia ni mbunge wa Kawe, alisema baraza hilo limeamua kuitisha maandamano hayo ili kuwakilisha kilio cha wanawake ambao ndiyo waathirika wa kwanza pale nchi inapokuwa katika mfumo usio wa haki.
Alivitaka vyombo vya dola hasa polisi kujitokeza kuwasindikiza na kuandamana nao kwa kuwa nao ni miongoni mwa Watanzania ambao wataathiriwa na uamuzi usiolenga kujenga umoja wa kitaifa.
Hata hivyo, Polisi imetahadharisha kuwa itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria wanachama wa Chadema watakaojiingiza katika maandamano yaliyopigwa marufuku nchini.
Msemaji wa Polisi, Advera Bulimba alisema, “Kauli yetu haijabadilika, maandamano ya Chadema ni batili. Yeyote atakayeandamana atakuwa anakiuka utii wa sheria bila shuruti. “Jukumu letu ni kuwalazimisha wote wasiotaka kufanya hivyo, kuitii kwa shuruti.”
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhaj Mussa Salum amewataka Watanzania kutokuwa na papara ya kupata Katiba Mpya kwani mwisho wa siku wenye uamuzi wa kutaka iwe ya namna gani ni wao.
“Ni vyema na busara Watanzania wakasubiri na kuliachia kazi Bunge hilo Maalumu ambalo linamaliza kazi hivi karibuni na wao kubaki na kazi ya kuchagua wanachokitaka kiwemo kwenye katiba hiyo.
Maandamano yazimwa
Polisi wamedhibiti wafuasi wa Chadema maeneo mbalimbali waliokuwa wamejipanga kufanya maandamano na wengine wamefikishwa kortini.
Wanachama zaidi ya 40 wa Chadema eneo la Mbalizi, Mbeya Vijijini walikumbana na virungu vya polisi muda mfupi baada ya kuanza maandamano katika Mtaa wa Z.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alisema hakuwa na taarifa yoyote lakini angependa wakazi wa Mbeya wafikirie zaidi masuala ya elimu, biashara na kilimo kuliko siasa.
Katavi
Viongozi watatu na wafuasi 14 wa Chadema Mkoa wa Katavi wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufanya maandamano bila kibali.
Wanachama hao walikamatwa jana saa nne asubuhi eneo la Zahanati ya Kasimba katika Mtaa wa Majengo A, wakiwa wanaandamana kwenda Viwanja vya Hoteli ya Mpanda walikopanga kufanya mkutano.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema wanaoshikiliwa ni: Katibu wa Chadema wa Mkoa, Almasi Ntije, Mwenyekiti Wilaya ya Mpanda, Abraham Mapunda na Katibu wa Jimbo la Mpanda Mjini, Cretus Nkumba.
13 wanaswa Mwanza
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola amesema wanawashikilia watu sita baada ya kukutwa wamejikusanya katika makundi jambo lilioashiria walitaka kuandamana.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mwanza, Adrian Tizeba alisema wanaoshikiliwa ni wanachama 13 na viongozi wao. Aliwataja baadhi ya viongozi wanaoshikiliwa kuwa ni Mwenyekiti wa Chadema Vijana Mkoa, Joseph Idd, Mwenyekiti Wilaya ya Nyamagana, Josephat Nungwana na Katibu wa Vijana Wilaya ya Ilemela ambaye hakumtaja.
Dar es Salaam
Wafuasi 12 Chadema wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka ya kufanya mkusanyiko usio halali kwa nia ya kuandamana.
Wakili wa Serikali, Bernard Kongola aliwataja washtakiwa hao mbele ya Hakimu Mkazi, Frank Moshi kuwa ni Paulo Stanley ‘Ndege’, Joseph Michael, Ajenta Emmanuel na Waziri Saidy ‘Mahunzi’.
Wengine ni Oldgard Lerio, Sifa Majura, Magreth Mapunda, Remina Peter, Stella Masanja, Mwanahamisi Hassani, Vaileth Seka na Sina Manzi.
Kongola alidai mahakamani kuwa juzi katika maeneo ya Ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ilala Boma walifanya mkusanyiko usio halali kwa nia ya kuandamana kinyume cha sheria.
Baada ya kusomewa mashtaka yanayowakabili, washtakiwa wote walikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Washtakiwa hao walirudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana na kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 8.
No comments:
Post a Comment