Askofu
mpya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya
Ziwa Tanganyika, Ambele Mwaipopo ametaka kusitishwa kwa mchakato wa
uundwaji wa Katiba Mpya kwa kuwa Bunge la Katiba limepuuza maoni ya
Watanzania yaliyowasilishwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba.
Askofu Mwaipopo
alisema hayo jana kwenye ibada ya kusimikwa kuwa askofu wa kanisa hilo,
katika Kiwanja cha KKKT, Usharika wa Sumbawanga Mjini, iliyohudhuriwa
viongozi mbalimbali akiwamo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
“Tusione aibu
kujikosoa kama tumekosea...zoezi hilo lisitishwe ili tujipange upya
lakini kuendelea kupuuza maoni ya Watanzania itatugharimu,” alisema
Askofu Mwaipopo huku akishangiliwa na waumini.
Alisema kanisa hilo
litaendelea kuwahamasisha wananchi kujiandikisha katika daftari la
kudumu la wapiga kura ili waweze kusaidia kupatikana kwa viongozi wenye
nia ya kuboresha maisha yao na kuondoa wanaosababisha umasikini.
“Nchi hii ni
tajiri, ina rasilimali nyingi, umasikini unatokana na kuwa na viongozi
wanaojijali wenyewe badala ya kuangalia maisha ya Watanzania wote...sasa
tutahakikisha tunahamasisha wananchi kujiandikisha kwenye daftari la
wapiga kura ili watuchagulie viongozi safi,” alisema.
Awali, Askofu Mkuu
wa kanisa hilo, Dk Alex Malasusa alitaka viongozi wa Taifa kubadilika na
kuwa na dhamira ya kutenda kile wanachokizungumza kwa kuwa wamekuwa
mabingwa wa kuongea kuliko kutenda.
Dk Malasusa alisema
viongozi wamekuwa mstari wa mbele kuzungumzia rushwa wakati hawana
dhamira ya kupambana nayo, hivyo imefika wakati matendo yao yaendane na
kauli zao.
Kwa upande wake,
Waziri Mkuu Pinda alisema mchakato wa uundwaji wa Katiba Mpya unaondelea
ni halali kwa kuwa Bunge hilo lipo kisheria na haliwezi kusitishwa,
kinachofanyika ni kuboresha yaliyomo kwenye Rasimu iliyowasilishwa kwao.
“Walioandaa ile Rasimu ni binadamu kama sisi, kuna mambo mengi waliyasahau, sasa tunayaboresha.
“Hatuwezi kupitisha
vilevile ile Rasimu, wananchi wangetushangaa kulikuwa na upungufu
mwingi kama kwenye ardhi, haki za binadamu na za walemavu,” alisema
Pinda.
Alisema kama tatizo
ni muundo wa muungano anafikiri kuna haja ya wananchi kupiga kura ya
maoni kama wanataka muungano wa aina gani.
No comments:
Post a Comment