Rais wa
Marekani Barrack Obama ametangaza mpango wake wa kuwatuma wanajeshi
3,000 Afrika Magharibi kama njia mojawap ya kusaidia katika vita dhidi
ya ugonjwa hatari wa Ebola.
Rais Obama ametoa wito kwa jamii ya
kimataifa kuchukua hatua za dharura kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Ebola
Magharibi mwa Afrika ambao unaenea kwa kasi sana.Bwana Obama amesema kuwa iwapo mlipuko wa maradhi hayo haukomeshwi kwa sasa, mamia ya maelfu ya watu wataambukizwa na yatakuwa tishio kwa usalama wa dunia.
Jemedari mmoja wa Marekani amewasili nchini Liberia kuongoza wanajeshi hao 3,000 wa jeshi la Marekani waliotumwa eneo hilo kupambana na maradhi hayo.
Wanajeshi hao watasimamia ujenzi wa vituo vipya vya kimatibabu na pia watahusika katika utoaji wa mafunzo ya kimatibabu kwa wahudumu.
Kumekuwa na malalamishi kwamba jamii ya kimataifa imelegea katika harakati za kukabiliana na mkurupuko wa Ebole katika mataifa ya Afrika magharibi.
Mataifa ya Sierra Leone, Liberia na Guinea ndiyo yaliyoathirika zaidi huku zaidi ya watu 2,400 wakiwa tayari wamepoteza maisha yao kufikia sasa.
Zaidi ya nusu ya idadi ya watu waliofariki kutokana na ugonjwa huu ni raia wa Liberia.
Shirika la afya duniani (WHO) limetahadharisha kuwa huenda watu zaidi wakazidi kufariki.
Umoja wa Mataifa (UN) unapangiwa kuzungumzia jinsi ya kukabiliana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika mkutano unaopangiwa kufanyika huko Geneva.
No comments:
Post a Comment