UTAFITI uliofanywa na mradi wa PREPARE uliokuwa na lengo la kuangalia uwezekano wa vijana kupunguza ngono, umebainisha elimu ya afya ya uzazi bado inahitajika ili kuwakinga na tabia hatarishi.
Akitoa matokeo ya awali ya utafiti huo, mmoja wa watafiti wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili, kitengo cha magonjwa na afya ya akili, Lusajo Kajula, alisema kuwa asilimia 10 ya vijana wenye umri wa miaka 12 hadi 14 ambao ni wanafunzi wa darasa la tano na sita wameshawahi kufanya ngono.
Alisema ngono hiyo kwa asilimia kubwa hufanywa na wanafunzi hao kinyume na maumbile.
Kajula alisema vijana wengi wamebainika kufanya ngono ya kawaida na ya mdomo, ikifuatiwa na ngono ya kinyume na maumbile.
Alisema kwa wale ambao wameshawahi kufanya ngono, asilimia 6.3 wamefanya kinyume na maumbile wakati asilimia 93.7 hawajawahi kufanya.
Alisema utumiaji wa kondomu umebainika kuwa mdogo kwa vijana wadogo ambao wameanza kufanya ngono.
“Asilimia 68 ya wale walioanza kufanya ngono hawajawahi kutumia kondomu kabisa, wakati asilimia 32 wamewahi kutumia,” alisema.
Alisema hiyo ni sehemu ya utafiti wa miaka minne ulioshirikisha Chuo Kikuu cha Makerere cha Uganda, Cape Town na Limpopo vya Afrika Kusini, Bergen na Oslo vya Norway, Maastricht cha Uholanzi na Sussex cha Uingereza.
Katika utekelezaji wa utafiti huo, wanafunzi 5,099 walichaguliwa mwanzoni mwa mradi kufanyiwa utafiti huo, ambapo 4,783 (asilimia 93.9) walifuatiliwa kwa miezi 6 na wengine 4,370 (asilimia 85.8) kwa miezi 12.
Mradi huo wa PREPARE ulitekelezwa kwenye shule 38 kutoka Manispaa ya Kinondoni zilizochaguliwa, kwa kutumia sampuli mtawanyiko, zilizopangwa katika makundi mawili ya shule.
“Kimsingi tunataka kuwaambia wanahabari kuwa miongoni mwa mafanikio makubwa ya mradi wa PREPARE ni kuchelewesha kuanza ngono miongoni mwa wanafunzi wa kiume na wa kike wenye umri wa miaka 12-14 katika Mkoa wa Dar es Salaam,” alisema Kajula.
Matokeo yaliyotathminiwa ni mabadiliko katika masuala ya ngono (kuanza ngono) na kutumia kondomu wakati wa kujamiiana kwa wale waliokwishaanza vitendo hivyo.
Kajula alisema kwa wastani mradi wa PREPARE umefanikiwa kupunguza uwezekano wa vijana wadogo hasa wavulana na wasichana kuanza ngono na kuongeza matumizi ya kondomu kwa wale walioanza.
Hata hivyo, katika utekelezaji wa mradi mabadiliko katika uchukuaji wa hatua yalionekana zaidi miongoni mwa wasichana waliopata mwingilio ukilinganisha na wale ambao hawakupata.
Alisema uchukuaji wa hatua ulisababisha kuwapo tabia ya kutumia kondomu kwa wanafunzi wa jinsia zote na taarifa za ongezeko la utumiaji wa kondomu miongoni mwa vijana wa kiume.
Kajula alisema ili kuweza kupata matokeo yaliyokusudiwa, mradi ulitoa mafunzo kwa walimu watano wakufunzi wa wakufunzi.
Alisema mradi ulitoa mafunzo kwa walimu watekelezaji 76, na waelimishaji rika wanafunzi 132 na kuelekeza watoa huduma 8 wa afya katika kliniki za huduma rafiki kwa vijana ili kutekeleza mwingiliano.
Mradi huo umefadhiliwa na Umoja wa Nchi za Ulaya, ambapo programu ya utafiti wa afya imelenga kuangalia mwingilio ulio katika misingi ya utamaduni na jinsia, endelevu, kijamii ili kukuza ujinsia na afya ya uzazi miongoni mwa vijana wenye umri miaka 12-14 kwa kutumia shule kama njia ya kufundishia.
Mtathmini kiongozi wa mradi huo, Mrema Kilonzo, alisema utafiti umeonyesha haja ya kutolewa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana wadogo ambao bado hawajaanza ngono ili kuchelewesha kuanza ngono kwa mfumo wa kisaikolojia kama njia ya kufanya wajitambue.
No comments:
Post a Comment