Tuesday 21 October 2014

ALIYEUAWA NA KOMANDOO WA JWTZ MSIBA WAKE WAZIZIMA


INAUMA sana! Baadhi ya ndugu waliokuwa wakiuaga mwili wa Aron Kihundwa (28) kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar walijikuta wakidondoka na kuzimia kufuatia uchungu wa kumpoteza mpendwa wao huyo aliyedaiwa kuuawa na Komandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Octavian Mgowele.
Aron Kihundwa akiwa mahututi hospitali kabla ya kifo chake.
Tukio hilo lilijiri wiki iliyopita na kumfanya Mchungaji  Elaina Msuya wa Kanisa la KKKT aliyekuwa akiongoza misa ya kumuombea marehemu huyo, kuingilia kati na kusema mwili usiendelee kuagwa ili kuzuia watu kuzidi kuzimia.
Komandoo Octavian Mgowele mwenye cheo cha Luteni wa Kikosi cha 94 KJ Ngerengere, Morogoro, Oktoba 13, mwaka huu alidaiwa kumuua Aron kwa kumpiga kipigo kibaya.Tukio hilo lilidaiwa kutokea kwenye baa iitwayo Mbondela iliyopo Yombo - Buza maeneo ya Kipera, jijini Dar kwa madai kwamba alikuwa akimbughudhi mke wa komandoo huyo.
Taarifa toka kwa mtu aliyekwepo kwenye baa hiyo zinasema siku hiyo mjeshi huyo alikaa meza moja na mkewe ambaye alitoka kufunga naye ndoa jana yake. Pia kwenye meza hiyo  alikaa Aron huku wakiendelea kunywa bia ambapo mnunuaji mkuu alikuwa komandoo.
Marehemu Aron Kihundwa enzi za uhai wake.
Ikadaiwa kuwa, kuna wakati komandoo alikwenda kaunta aliporudi alishangaa kumkuta mkewe amehama katika kiti alichomuacha.Chanzo hicho kikaendelea kusema komandoo huyo alimuuliza mkewe kisa cha kuhama kiti, naye akamjibu; si huyu rafiki yako ananisumbua.’
Wakati huo, marehemu alikuwa anauchapa usingizi kutokana na kulewa.
“Marehemu akiwa usingizini alishtukia komandoo akimwadhibu bila kujua sababu ni nini hadi akamjeruhi.
”Baada ya kumpiga sana hadi kumjeruhi tulimchukua marehemu na kumpeleka Kituo cha Polisi Chang’ombe (Dar) na kupewa PF3, tukamkimbiza Hospitali ya Temeke,  ilipofika saa kumi usiku wa kuamkia kesho yake alifariki dunia.
“Aron ni rafiki yake sana komandoo, hata siku ya ndoa yake, yeye ndiye aliyempambia gari la harusi na ukumbi. Siku ya tukio ilikuwa ni sherehe ya kuvunja kamati.
“Hatujajua ni kwa nini komandoo aliamua kumpiga Aron kiasi kile, mambo ya kuambiwa na mwanamke siyo ya kuyafanyia kazi kama haukushuhudia ama hauna uthibitisho,” alisema shuhuda huyo.
Marehemu Aron alizikwa Oktoba 18, mwaka huu kijijini kwao Kyengia Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.

No comments:

Post a Comment