Tuesday 14 October 2014

MKUU WA WILAYA YA KOROGWE APANDISHWA KIZIMBANI KWA TUHUMA ZA KUTUMIA LUGHA YA MATUSI NA KASHFA




Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Mrisho  Mashaka Gambo jana amefikishwa mbele ya Baraza la Maadili ili kujibu tuhuma zinazomkabili.

Akisoma hati ya malalamiko yanayomkabili  Mhe. Gambo, Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Hassan Mayunga alisema kuwa Mhe. Gambo amekuwa akitumia lugha ya matusi  na kashfa dhidi ya watumishi wa Halmashauri ya Mji  Korogwe kinyume na Misingi ya Maadili ya Viongozi kwa mujibu wa fungu la 6 la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma sura (398).

Pia, Mhe. Gambo analalamikiwa kuwa aliweka shinikizo kwa Halmashauri ya Mji wa Korogwe kukiuka Taratibu za Manunuzi ya Umma kinyume na matakwa ya fungu la 6 (c ) linalomtaka Kiongozi wa Umma kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria.

Aidha, lalamiko lingine linalomkabili Mhe. Gambo ni  kuweka shinikizo lisilofaa kumuhamisha Mtumishi wa Umma kinyume na fungu la 12 (1) (c) la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, sura 398. 

Hata hivyo Mhe Gambo alikana malalamiko yote yaliyowasilishwa mbele ya Baraza dhidi yake na Shauri lake limeahirishwa mpaka tarehe 15 Oktoba, 2014 ambapo Baraza litapata fursa ya kusikiliza ushahidi kutoka upande wa Mlalamikiwa baada ya leo kuanza kusikiliza ushahidi kutoka upande wa Walalamikaji.

Awali Baraza la Maadili lilianza kusikiliza shauri linalomkabili Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora Bibi Sipora J. Liana ambaye wakati akifanya makosa alikuwa ni Mkurugenzi wa Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani.

Akisoma hati ya malalamiko, Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bibi Getrude Cyriacus alisema kuwa Mlalamikiwa bila sababu za msingi na bila kufuata utaratibu alimchukulia hatua za nidhamu kwa kumsimamisha kazi Dkt. Francis Malya aliyekuwa Afisa Kilimo, Mifugo na Ushirika wa Wilaya ya Mkuranga kinyume na fungu la 12 (c) la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995.

Bibi Cyriacus aliendelea kumsomea malalamiko mengine Mlalamikiwa ambayo ni Mlalamikiwa bila kufuata taratibu alifuta hoja za ukaguzi za robo ya nne ya mwaka 2009/2010 kwa kumuagiza aliyekuwa mhasibu Bw. Shabani Yusuph kufanya hivyo kinyume na matakwa ya Sheria ya Fedha ya 2004 pamoja na Mlalamikiwa kutumia wadhifa wake kujinufaisha kinyume na fungu la 12 (1) la Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995 kwa kukiuka taratibu za Manunuzi katika Serikali za Mitaa za mwaka 2007 kwa kutafuta yeye mwenyewe na kuwalipa fedha wazabuni ambao hawakupitishwa na Bodi ya Zabuni.

Maelezo ya malalamiko yaliyosomwa na Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bibi Getrude Cyriacus yalifuatiwa na kusikilizwa kwa ushahidi kutoka upande wa Walalamikaji uliotolewa na Dkt. Francis Malya ambaye alilieleza Baraza la Maadili namna Bibi Sipora Liana alivyoshiriki kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa umma na kutoa vielelezo mbalimbali ili kuweza kulilidhisha Baraza hilo ukweli wa maelezo yake.

Hata hivyo Mlalamikiwa alikana tuhuma zote dhidi yake na kuomba nafasi ya kuitwa mashahidi wake mbele ya Baraza ili nao wapewe nafasi ya kutoa maelezo kuhusu shauri hilo ambapo Baraza hilo lilimkubalia ombi lake na Shauri lake liliahirishwa mpaka tarehe itakayotangazwa hapo baadae.

Wakati huo huo, Mkurugenzi Msaidizi - Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bibi Sara Kinyamfura Barahomoka amejisalimisha mbele ya Baraza la Maadili baada ya kutolewa agizo la kukamatwa baada ya kukaidi wito wa kufika mbele ya Baraza  tarehe 10 Oktoba, 2014 kujibu tuhuma zinazomkabili.
Hata hivyo  Mwenyekiti wa Baraza hilo Mhe. Jaji (Mst.) Hamis Msumi alimpa onyo kwa kosa hilo na kuahirisha kusikiliza shauri lake mpaka tarehe 15 Oktoba, 2014 ambapo litaanza kusikilizwa kwa mara ya kwanza.https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEh490x6YhwvJ6YMXPR8D4hQ-Q8vy3EuNNF-aTZGZCpWr5PInbKr5yh700vO6ZMlXn8hyphenhyphenhtPJMfewPpVnYrwdTGU7Iu4k40enxkT4ZbvKG5KjLUCm2IRtAX37d_q-M4i_K9AfbzL0MauIi2p/s1600/unnamed.jpgMwenyekiti wa Baraza la Maadili Mhe. Balozi Jaji (Mst.) Hamisi Msumi katikati akiwa na Wajumbe wa Baraza hilo Bibi Selina Wambura kushoto na Bibi Hilda Gondwe kulia kabla ya kuanza kusikiliza Mashauri ya ukiukwaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma yaliyowasilishwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

No comments:

Post a Comment