NI BAADA YA MECHI 13 NA SUNDERLAND TU!!
Sunderland wamemtimua Meneja wao Paolo Di Canio baada
ya mwanzo mbovu kwenye Ligi Kuu England ambapo Timu hiyo imejikuta ipo mkiani
kwenye Msimamo wa Ligi hiyo.
Tangu ateuliwe kuwa Meneja wa Sunderland Mwezi Machi,
Di Canio, mwenye Miaka 45, ameshinda Mechi 3 tu kati ya 13 alizosimamia na
Msimu huu ameambua Pointi 1 tu katika Mechi 5 za Ligi.
Klabu ya Sunderland imetoa tamko kuwa mrithi wa Di
Canio atatangazwa hivi karibuni na kwa sasa Timu hiyo itakuwa chini ya Kocha
Kevin Ball.
WASIFU WA PAOLO DI CANIO:
-KUZALIWA:
Rome, 9 Julai 1968
-KLABU ALIZOCHEZA:
Lazio, Juventus, Napoli, AC Milan, Cisco Roma, Celtic,
Sheffield Wednesday, West Ham, Charlton
-FAINI:
£10,000 Mwaka 1998 kwa kumsukuma na kumwangusha Refa
Paul Alcock baada ya kutolewa katika Mechi dhidi ya Arsenal
-TUZO YAUCHEZAJI WA HAKI:
Mwaka 2001 kwa kudaka Mpira badala ya kufunga ili Kipa
wa Everton Paul Gerrard apate Huduma ya Kwanza baada ya kuumia.
-APONDWA:
Mwaka 2005 kwa kutoa Saluti ya Kifashisti kwenye Gemu
na Lazio.
-ATEULIWA:
Bosi wa Swindon Mei 2011 na kuwapandisha LIGI 1 Mwaka
mmoja baadae
-AJIUZULU:
Kama Bosi wa Swindon Februari 2013
-AMBADILI:
Martin O'Neill kama Meneja wa Sunderland Machi2013 na kuinusuru
kushushwa Daraja toka Ligi Kuu England.
-ATIMULIWA:
Sunderland baada Mechi 5 za Ligi ambazo amefungwa 4
kati ya hizo na Sare moja.
Mechi ya kwanza chini ya Kocha Kevin Ball itakuwa ni leo
watakapocheza Nyumbani Stadium of Light na Peterborough United kwenye Raundi ya
Tatu ya Capital One Cup.
Baada ya Mechi hiyo, Sunderland watakuwa Wenyeji kwa
Liverpool Jumapili ijayo, kisha kucheza na Manchester United Oktoba 5 na
kufuatia Dabi ya eneo la Wear-Tyne dhidi ya Newcastle hapo Oktoba 27.
Mwezi Machi Mwaka huu, Di Canio alitinga Sunderland
kuchukua nafasi ya Martin O'Neill, aliefukuzwa na akakaribishwa na madai kuwa
yeye anasapoti Mafashisti.
Meneja huyo kutoka Italy mwenye vituko amekuwa mwepesi
kuwaponda Wachezaji wake waziwazi Magazetini na hili limeleta mkwaruzo ndani ya
Timu.
Mbali ya kusaini Wachezaji 14 kwa ajili ya Msimu huu
mpya, Di Canio pia aliwauza Wachezaji mahiri Kama Kipa Simon Mignolet kwa
Liverpool na Stephane Sessegnon kwa West Brom ambae hivi Juzi katika Mechi yake
kwanza tu na West Brom alifunga Bao walipoicharaza Sunderland 3-0.
Sunderland sasa inasaka Meneja mpya wa 6 katika
kipindi cha chini ya Miaka mitano.
HABARI toka ndani ya
Sunderland zimesema kuwa Wachezaji Wakongwe wa Klabu hiyo walimkabili
Mkurugenzi Mtendaji Margaret Byrne na kulalamika kuhusu Paolo Di Canio kabla
hajafukuzwa kama Meneja wao.
Mara baada ya kufungwa
na West Brom 3-0 hapo Jumamosi, Siku ya Pili Di Canio alifanyiwa Mkutano na
Wachezaji ambao unadaiwa cheche ziliwaka.
Baadae ndio Kundi hilo
la Wachezaji Wakongwe likamfuata Mkurugenzi Mtendaji na kumwambia kuwa Mtaliana
huyo hawezi kubaki kwani himaya yake ni ya Kikatili na mbovu kwa kuwaponda
Wachezaji hadharani.
Miongoni mwa wanaotajwa
kuchukua nafasi hiyo ni Meneja wa zamani wa Chelsea Roberto Di Matteo na
wengine ni Gus Poyet, Tony Pulis na Alex McLeish.
Wakati huohuo
Meneja wa sasa wa Hull
City - Steve Bruce amedai kuwa Paolo Di Canio staili yake ya uongozi ndio
imemfukuzisha kazi ya Umeneja huko Sunderland.
Inaaminika staili ya
Di Canio ya kuwa mkali na kuwaponda Wachezaji wake hadharani ilileta
manung’uniko miongoni mwa Wachezaji na ni sababu kubwa iliyomfanya afukuzwe.
Steve Bruce, ambae
aliwahi kuwa Meneja wa Sunderland kati ya Mwaka 2009 na 2011, amesema: “Huwezi
kuwa Meneja wa Klabu ya Ligi Kuu siku hizi huku ukiongoza kwa kutisha Watu.
Kuongoza Watu vizuri ni muhimu kuliko hata kufundisha Soka. Ukiwa Ligi Kuu
Wachezaji wote ni wazuri na kilichobaki ni kuwafanya wacheze vizuri zaidi.
Huwezi kuongoza kwa kuponda Watu hadharani. Namwonea huruma. Meneja amepoteza
kazi. Utawala ni kazi ya upweke na amepoteza kazi. Nimewahi kupitia hilo na si
kitu kizuri”
No comments:
Post a Comment