Sunday 7 September 2014

INSPEKTA WA JESHI LA POLISI AKAMATWA NA BUNDUKI MBILI ALIZOKUWA AKITUMIA KUWINDIA WANYAMA


Inspekta wa Jeshi la Polisi  ambaye pia alikuwa mtunzaji mkuu wa ghala la silaha za polisi Dodoma, George Nelson amekamatwa akiwa na bunduki mbili alizokuwa akizitumia kuwindia wanyama. 
Mbali na bunduki hizo, alipatikana akiwa na nyama ya swala anayedaiwa kuwinda kinyume na sheria na magunia sita ya mkaa.
 
Polisi huyo alikamatwa na kikosi maalumu cha Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) kinachoendesha operesheni kimya kimya ya kuwakamata watu wanaojihusisha na ujangili nchi nzima.

Habari za uhakika zilizothibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, David Misime zilieleza kuwa Inspekta Nelson alitiwa mbaroni Agosti 24, mwaka huu akiwa na Bunduki ya kivita G3  yenye namba G3FS 12v526. 
Bunduki hiyo iliyokuwa kwenye ghala la silaha la polisi Dodoma, ilikuwa na namba za usajili za ghala TZPL 12984 ikiwa na risasi 20 mali ya serikali.
 
Bunduki nyingine ni shotgun yenye namba za usajili 58433 yenye risasi tisa ambayo ilikuwa ikihifadhiwa kwenye ghala la polisi Dodoma kama kidhibiti.
 
Pamoja na Kamanda Misime kukataa kueleza kwa kina akidai ataingilia upelelezi unaofanywa na waliomkamata (Tanapa), lakini chanzo cha habari kilieleza kuwa Inspekta Nelson aliyekuwa na vijana watatu, Simon Mawala Gene (25) wa Miuji, Isack George (23) wa Chinangali na dereva Juma Ramadhani Mtawike (25) wa Maili Mbili wote kutoka mkoani Dodoma, alipatikana pia na nyama ya swala anayedaiwa kumuwinda bila kibali na magunia sita ya mkaa.
 
Habari zaidi zinaeleza kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa amebeba vitu hivyo kwenye gari dogo pickup nyeupe aina ya Suzuki yenye namba T 776 CHY.
Inspekta Nelson mkazi wa Polisi Line namba 48, Dodoma, ajira yake inaelezwa kukoma mwanzoni mwa mwezi wa nane baada ya kustaafu.

Pamoja na kustaafu huko, chanzo cha habari kilieleza kuwa alikuwa akiendelea kuchukua silaha kwa ajili ya uwindaji haramu.
 
Imeelezwa kuwa sakata la kukamatwa kwa Inspekta Nelson, limesababisha baadhi ya maofis wa ngazi za juu wa jeshi hilo kuhamishwa vitengo ikiwa ni pamoja na mmoja wa ngazi ya juu mkoani humo  kuhamishiwa Morogoro.
 
Hata hivyo, Misime pia alikataa kutoa ufafanuzi wa uhamisho huo akidai mwenye mamlaka ya kuajiri, kuhamisha na kuzungumzia uamuzi huo ni Mkuu wa Jeshi hilo.

No comments:

Post a Comment