Monday 22 September 2014

Maswali manne kwa Samuel Sitta na vyama vya siasa

Tanzania


Tusipoyauliza leo, hakika tutaulizwa sisi na vizazi vijavyo tukiwa hai au tukiwa tumetangulia mbele ya haki
Kabla ya kuuliza maswali yangu manne, ni vema nikaeleza kwanza sababu za msingi za kwanini ninauliza maswali haya muhimu. Ninauliza kwasababu ninaona hatuna uelewa wa pamoja juu ya mchakato huu, uelewa wa tumetoka wapi, kwanini tuko hapa na tunapaswa kwenda wapi. Yako maelezo mengi na yamesemwa mengi juu ya hasa kwanini tuliingia katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya, ikiwemo uthubutu na utashi wa kisiasa wa mkuu wa nchi kuuanzisha mchakato pamoja na msukumo wa miaka nenda rudi kudai Katiba Mpya kutoka mtu mmoja mmoja, asasi za kiraia na hasa vyama vya siasa.
Tumetoka wapi
Sote tuna uelewa wa pamoja kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliasisiwa Mwaka 1964 na kuunda Nchi Moja Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuna mazingira yaliyopelekea sisi kuungana na sababu za kuungana, ulinzi na usalama likiwa jambo kubwa zaidi wakati huo na kwa hakika hata kwa mazingira ya leo bado ile kauli mbiu ya umoja wetu ni Muungano wetu inabeba uhalisia wetu. Unapounganisha Nchi katika mazingira ya kushughulika na suala la ulinzi na usalama wa eneo husika hata mtindo wa kiutawala na kiuongozi huwa lazima uakisi mazingira hayo.
Baadhi yetu hatufuatilii historia na kudadisi sana, lakini huenda wengi wetu tunafanya hivyo, na hatushangai kwanini kwa miaka 13 baada ya Muungano (1964) ndipo Katiba ya kudumu iliandikwa mnamo mwaka 1977. Katiba hii ya kudumu inayoakisi uhalisia wa mazingira ya kipindi kile, sote tunakubaliana iliandikwa kwa uwakilishi na Watanzania kiuhalisia hawakuiandika na kuipa uhalali Katiba yao na ndiyo maana mwaka 1984 ilifanyiwa marekebisho makubwa na hata leo yameshafanyika marekebisho 14. Kwa hakika imetufikisha hapa lakini imekabiliwa na changamoto nyingi ambazo nyingine haziwezi kuondoka kwa kufanya marekebisho tu. Umefika wakati wa kujizaa upya.
Tuko wapi
Mwishoni wa mwaka 2010, Rais alituanzishia mchakato ambao kwa asili yake unapaswa kutupatia Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katiba hii mpya inaandikwa na Watanzania wenyewe na mchakato wake ukijumuisha mbinu madhubuti za ushiriki wa moja kwa moja na kupitia wawakilishi. Katika hatua nne kama zinavyobainishwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83, tuko katika hatua ya tatu ambayo ni Bunge Maalumu la Katiba, ambayo imekwisha tanguliwa na hatua ya kwanza, kukusanya maoni na hatua ya pili, kuboresha Rasimu ya Awali katika Mabaraza ya Katiba. Hatua itakayofuata itakuwa ni Kura ya Maoni.
Tulianza vizuri ukiacha changamoto za hapa na pale, hadi pale ndugu zetu wa vyama vya siasa walipoamua kuweka misimamo yao ya kichama na kutupilia mbali maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla. Katika kila ugomvi hasa wa kifamilia lazima tumpate mtu wa kumtwisha mzigo wa lawama, na ukizingatia sisi kama Taifa ni familia moja, basi ninaweza sema chama Tawala kinapaswa kuwa kimetoa uongozi katika mchakato huu. Dhamira ya Rais ilikuwa hatua moja, hatua ya pili ilikuwa kutafsiri dhamira hiyo ukizingatia nafasi ya vyama vya siasa katika michakato ya Katiba ulimwenguni kote ambayo huwa ni; moja, kujenga mwafaka, pili, kufanya maridhiano, tatu, kuhakikisha kuna uwakilishi makini na nne, kuhakikisha kuna nidhamu katika ushiriki (hasa kwa wafuasi wao). Haya mambo manne, nikisema kwa unyenyekevu na kwa kuwatendea haki, hayajafanyika kabisa, kimsingi wameyatupilia mbali. Ndiyo kwa maneno mengine mchakato huu umekwama sema tunalazimisha uonekane unakwenda, kwa ubabe ubabe.
Kwanini tuko hapa
Tumekwama, na jibu zuri la kwanini tumekwama, ni moja tu, kwamba masilahi binafsi ya watu, maslahi ya makundi hasa vyama vya siasa yanaonekana kufanya vizuri zaidi dhidi ya maslahi ya wananchi ambao kwa wingi wao walitoa maoni yao Tume ya Katiba. Jitihada zimefanyika kujaribu kuwaleta pamoja wadau hawa wakubwa wa Katiba na Demokrasia nchini na ama zilishindwa, ama hazijazaa matunda, ama zimepuuzwa au hatujaona dhamira ya kweli na utashi wa kutaka kukwamua mchakato huu uliokwama.
Katika jitihada za kukwamua niliona walianza watu wa Baraza la Vyama vya Siasa (TCD) pale mwanzoni, wakapotea. Walipo potea TCD muda si mrefu Bunge Maalumu likiendelea na tafrani zake vyama vitatu vikuu vya upinzani vikasusia vikao vya Bunge Maalumu, mpaka leo. Wakaja kujaribu viongozi wa dini, tena dini zote, wakaombwa wasubiri kwanza, hawa ni kama waliombwa wakae ndani kusubiri basi la usafiri, loh! Kumbe basi likaja na likaondoka, ni kama wameachwa kituoni, wameduwaa na kuvunjika mioyo, lakini nina uhakika bado wanatuombea. Kuna kipindi hata watu kutoka nchi jirani kwa kushirikiana na asasi za kiraia za hapa nyumbani walijaribu kutumia usuluhishi kama njia ya kutukwamua, nadhani waliambiwa jambo hili bado ni la ndani na tunalimudu wenyewe ndani.
Baadaye akaja Msajili wa vyama vya siasa, akaenda, akaenda na muda si muda kupitia magazeti tukaarifiwa kwamba na yeye ameshindwa. Sasa TCD wamerudi na wakamzonga Rais kwamba aonane nao, wakaonana naye na baada ya vikao na Rais kwisha, walipotoka tu kila mtu anasema lake. Hawa ni watu ambao tunapaswa kufikiri mara mbili kuweka imani yetu kwao kwa asilimia zote, nashawishika kusema tukae nao macho.
Hawa watu ni wagumu kweli, ni wabishi kweli, ni majabali hakika na ni kama wana misimamo ya kufa na kupona na hawapendi hata kuijadili kwa uwazi, kwa hoja na sababu. Hawa wana hasira kweli, hawaoni haya kutusi watu hadharani, ila katika kipindi chote nimejifunza kwamba watu hawa wana mazuri yao pia.
Niulize ni yepi? Majabali haya unaweza kukaa nayo faragha mkateta hata kwa saa nyingi, kwanza ni wasikivu mkiwa katika vikao vya faragha, wanauliza maswali, wanaonekana wana hofu (hii ni ishara ya ubinadamu) na ukiwajibu hoja zao zote, hawaoni haya kukuunga mkono na kusema umesema kweli.
Ila nimejifunza majabali binadamu hawa huwa kana kwamba kuna jitu nyuma yao, jitu kubwa kuliko jabali, jitu nene, na lenye kutisha, huenda pua zake hupumua moto na moshi mwingi. Kwanini nasema hivyo, kwasababu majabali binadamu hawa huwa hawako tayari kukiri ukweli mbele ya umma, wengine wengi tu wameniambia kama tutafanya maamuzi kwa siri kwa hakika tutaunga mkono Rasimu ya Katiba Toleo la Pili. Bado namtafuta jitu.
Tunapaswa kwenda wapi
Kimsingi tunapaswa kupata Katiba Mpya ya Watanzania ambayo imetokana na maoni ya wananchi na ambayo ni tunda au tokeo la muafaka wa kitaifa, maridhiano na uelewa wa pamoja wa misingi ya kwanini tangu mwanzo tuliamua kuwa na Katiba Mpya. Kila Mtanzania mwenye mapenzi mema na Taifa lake anapaswa kung’ang’ania hapo bila kukata tamaa, maana kwa hakika haki husimama milele na kweli hutuweka huru daima kama mtu mmoja mmoja, taasisi na taifa la Tanzania kwa ujumla.
Swali la Kwanza (Kwa Vyama vya Siasa)
Je, kule kwenye majadiliano yenu na Rais mlikubaliana nini? Labda nikisie, mlikubaliana kusitisha mchakato kwa ujumla wake kwa kuwa mmeshindwa kukubaliana, kujenga mwafaka, kufanya maridhiano na kuwa na uelewa wa pamoja. Sasa kwanini Mwenyekiti wenu Cheyo anasema vingine na amebariki Sitta kuendelea na vikao vya Bunge Maalumu hadi Katiba Inayopendekezwa ipatikane?
Au ni Viwango na Kasi za Mzee wetu Samuel Sitta Mwenyekiti wa BMK ndiyo vinatugharimu sasa? Eti si mnajua tunaenda kufanya marekebisho ya 15 ya Katiba ya 1977, ninyi UKAWA mnasema mnataka mambo manne, mbona nimesikia Tanzania Kwanza wanataka mambo 17, je, mnajua tafsiri yake?
Swali la Pili (kwa Vyama vya Siasa)
Nikisie tena, labda kweli mlikubaliana kwamba Bunge Maalumu liendelee na tupate Katiba Inayopendekezwa tarehe 4 Oktoba 2014. Nauliza, yale masuala yooote ambayo hayajapata mwafaka kama ambavyo Katibu Mkuu Kiongozi amekiri jana kwenye gazeti la Mwananchi Jumamosi kwamba suala la Muundo wa Muungano hatujaweza kufanya maridhiano ila tunalazimishana, hayo masuala likiwemo la Muungano, je, ninyi vyama vya siasa hasa Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi mmeshakubaliana na CCM kwamba ni hizi Serikali Mbili “zilizo boreshwa”.?
Msipepese macho nataka mnijibu, tena mnijibu na kama mmeshakubaliana juu ya Tunu, Malengo Makuu, Maadili na Miiko, Muundo wa Serikali, Muundo wa Bunge, Wananchi kumwajibisha Mbunge, Ukomo wa Ubunge na Mapato ya Serikali ya Muungano. Wakurya wanasema kwa lafudhi yao “Chibuni Hocha kwa Hocha” wakimaanisha Jibuni hoja kwa hoja.
Swali la Tatu (Kwa Samuel Sitta)
Naomba kukuuliza wewe na Samia Suluhu akipata muda anaweza kunijibu pia, eti, ni nini ndoto yenu baada ya kuliongoza Bunge letu Maalumu ambalo mpaka sasa sisi tulio nje tunaona limeshindwa kujenga mwafaka wa kitaifa na limeshindwa kufanya maridhiano juu ya masuala nyeti ya Taifa letu.?
Naomba kuuliza swali la uchokozi kidogo ila mnisamehe maana si mnajua mimi ni kijana wenu tu, kwanini hamkumwita hata mara moja, hata kwa kumweka kiti moto Mwenyekiti wa Tume ya Katiba Jaji Joseph Sinde Warioba ambaye alileta Rasimu ambayo inaonekana kufanikiwa kuligawa Bunge Maalumu ambalo wewe na Samia Suluhu mnaliongoza kwa umahiri mkubwa?
Swali la Nne (Kwa Samuel Sitta)
Eti Sitta nini siri ya Mafanikio ambayo umeitumia kumaliza Bunge Maalumu tarehe 4 Oktoba 2014 mkiwa na Katiba Inayopendekezwa mkononi ilhali mwanzoni ulisema muda hautoshi kabisa? Suluhu, Makamu Mwenyekiti anaweza kunisaidia majibu ya nyongeza pia.
Maswali haya vizazi vijavyo vitayasoma na itapendeza kama majibu yenu tukiyapata mapema katika kizazi chetu. Na niwatakie kazi njema, nina shauku ya kuisoma Katiba Inayopendekezwa siku chache zijazo.
Itaendelea wiki ijayo
credits:mwananchi



No comments:

Post a Comment